Obama azungumza pia na Morsi na Erdogan
Aidha, Rais Obama amempongeza Rais wa Misri, Mohamed Morsi kwa juhudi ya kusaidia kuituliza hali kati ya Israeli na Gaza na kusisitiza matumaini yake ya kurejea kwa utulivu kwenye eneo hilo. Akizungumza na Morsi kwa njia ya simu, Rais Obama ameelezea umuhimu wa kumaliza mashambuliano haraka iwezekanavyo ili kuzuia maisha ya raia wasio ha hatia kupotea bila sababu. Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Kandil amesema nchi yake ipo tayari kupatanisha juu ya kusimamisha mashambiliano kati ya Israeli na Hamas. Misri ni mshirika wa Hamas, lakini pia imetiliana saini mkataba wa amani na Israeli mwaka 1979.
Rais wa Misri, Mohammed Morsi
Mbali na Netanyahu na Rais Morsi, Rais Obama amezungumza pia na Waziri
Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa njia ya simu ambapo kwa pamoja
wameelezea wasiwasi wao kuhusu hatari zinazowakabili raia wa pande zote
mbili na kuelezea nia yao ya kutaka kumaliza ghasia hizo. Taarifa ya
Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Obama na Erdogan pia wamesema
ghasia mpya katika Mashariki ya Kati zinahatarisha matarajio ya amani ya
kudumu katika eneo hilo.Mapigano yaendelea
Mazungumzo hayo kwa njia ya simu yamefanyika, wakati wapiganaji wa Hamas wakirusha maroketi kwenye miji ya Jerusalem na Tel Aviv jana Ijumaa. Israeli imesema imezifunga barabara zote kuu kuzunguka mpaka wake na Gaza, na kulielezea eneo hilo kama la kijeshi. Hatua hiyo ni ishara kwamba uvumilivu wa Israeli sasa umefikia kikomo na inajiandaa kuanzisha mashambulizi ya kwanza ya askari wa miguu katika eneo hilo tangu mwaka 2008 na 2009. Kiasi Wapalestina 21 na Waisraeli watatu wameuawa tangu Israeli ilipoanzisha mashambulizi siku ya Jumatano, wakati ilipomuua mkuu wa jeshi la Hamas, Ahmed al-Jabari.
Ban Ki-Moon azitolea wito Israeli na Hamas
Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon
amezitaka Israeli na Hamas kumaliza mashambulizi yanayoongezeka katika
Ukanda wa Gaza ili kuzuia mauaji zaidi katika Israeli na Palestina.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nersiky amesema Ban ana wasiwasi
mkubwa kuhusu kuendelea kwa ghasia kati ya Gaza na Israeli na anahofia
pia kupanda kwa gharama za maisha ya raia. Nersiky amesema Ban
anatarajiwa kuzuru eneo hilo hivi karibuni. Wanadiplomasia wa Umoja wa
Mataifa wamesema kuwa Ban atazuru Israeli na Misri wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment