Mhadhiri wa Kiislamu wa Kenya Aboud Rogo Mohammed, ambaye alikuwa
kwenye orodha ya kimataifa ya watu waliowekewa vikwazo kwa kuliunga
mkono kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda, alipigwa risasi
na kuuawa hapo Jumatatu (tarehe 27 Agosti) akiwa garini mwake mjini
Mombasa.
Mashahidi walisema kwamba gari hilo lilitobolewatobolewa kwa risasi.
Picha iliyosambazwa na wafuasi wake iliionesha maiti yake ikiwa imerowa
damu nyuma ya usukani wa gari.
"Alikufa wakati tukimuwaihisha hospitali," alisema mjane wake, Haniya
Said, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP kabla ya yeye mwenyewe na
watoto wake kupelekewa hospitalini.
Kifo cha Mohammed kilichochea maandamano ya maelfu ya waandamanaji
wenye hasira kukusanyika katika msikiti ambao alikuwa akiutumia kutoa
hotuba zake mara kwa mara, waliotia moto magari na kupiga mayowe ya
kumuunga mkono kiongozi huyo, iliripoti AFP.
"Imamu alipiga kelele kupitia spika ya msikitini "damu kwa damu", na
mara moja vijana wakaanza kuyarushia mawe magari," alisema shahidi
Dennis Odhiambo, ambaye gari yake iliathirika na akalazimika kukimbilia
kituo kimoja cha polisi kwa usalama wake.
Mkuu wa Polisi wa Mkoa huo, Aggrey Adoli, alisema: "Mtu mmoja ameuawa, alikatwa kwa mapanga hadi kufa wakati wa maandamano."
"Kuna vurugu mjini sasa, na maafisa wetu wako huko kuwatawanya waandamanaji kurudisha amani," alisema Adoli.
"Mji mzima uko kwenye hali mbaya, kuna waporaji mitaani, gari
zimevunjwa, mengine yamechomwa moto," alisema Francis Auma kutoka
Jumuiya ya Waislamu kwa Haki za Binadamu.
No comments:
Post a Comment