Wednesday, 18 July 2012
Polisi kuajiri askari wapya 3,000
JESHI la Polisi litaajiri askari wapya 3,000 wengi wao wakiwa wasomi kutoka taasisi za elimu ya juu.
Akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13 katika kikao cha Bunge, Dodoma jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema:
“Sehemu ya waajiriwa itapatikana kutoka katika shule na vyuo vya elimu ya juu na idadi nyingine kutoka vijana wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa). Utaratibu huu unalenga kuwa na askari wenye sifa stahiki na waaminifu kwa kazi ya Polisi.”
Alisema polisi wataendelea kuongeza ufanisi katika upelelezi wa makosa ya jinai na kwamba mwaka 2012/2013 litatumia vyuo vyake vya Dar es Salaam na Kidatu kutoa mafunzo kwa askari wa kufanya kazi hiyo.
Dk Nchimbi alisema mafunzo hayo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia na mbinu za kisasa za upelelezi, zitatolewa kwa maofisa, wakaguzi na askari wapatao 1,000.
Wakimbizi kurejeshwa makwao
Waziri huyo alisema Serikali inakamilisha taratibu za kuwarejesha makwao wakimbizi wapatao 40,000, wengi wao kutoka Burundi, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, Tanzania ilikuwa na wakimbizi 112,645 wakiwamo Warundi 48,195, Wakongo 62,632, Wasomali 1,548 na wakimbizi wa mataifa mengine 270.
Hatua ya kuwarejesha makwao wakimbizi itawezesha kufungwa kwa Kambi ya Mtabila, Kigoma yenye wakimbizi 38,800, ambayo inapaswa kuwa imefungwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
“Katika mwaka 2011/12, idadi ya wakimbizi wa Burundi kutoka kambi hiyo waliorejea kwao ni 155 tu, hali iliyosababisha kambi hiyo kutofungwa,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Mkakati mpya wa kufunga kambi hiyo ni kwamba limefanyika zoezi la mahojiano ya kina na wakimbizi hao kwa lengo la kubaini kama wapo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini.”
Alisema mahojiano hayo yalifanyika kati ya Septemba na Desemba mwaka jana na kwamba matokeo yanaonyesha kwamba 33,705 hawana sababu za msingi za kuendelea kuwa wakimbizi na wengine 2,045 walionekana kuwa na sababu za msingi.
Malumbano yaendelea
Malumbano yameendelea kulitikisa Bunge baada ya jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), William Lukuvi kukatisha hotuba ya Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Vicent Nyerere akidai inazungumzia mambo ambayo yako Mahakamani.
Nyerere alisoma bajeti yake baada ya ile iliyosomwa na Waziri Nchimbi lakini, wakati akiendelea, Lukuvi aliomba mwongozo wa Spika, Anne Makinda na kisha kuomba hotuba hiyo isitishwe.
Kitendo hicho kilisababisha mabishano ya kikanuni huku wabunge wakitunishiana misuli na kushindana kwa utaalamu wa kujua vifungu vya sheria na kanuni za Bunge.
Hii ni mara ya pili kwa Serikali kuzuia hotuba za wizara hiyo kutoka Kambi ya Upinzani. Mara ya kwanza ilikuwa katika hotuba ya Makadirio ya Mwaka jana (2011/12) ambapo aliyekuwa Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Godbless Lema alizuiwa kusoma hotuba yote.
Jana, baada ya Waziri Lukuvi kuwasilisha ombi lake, alisimama Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alisema haikuwa haki kwa Serikali kukatisha hotuba hiyo kivuli na kwamba kitendo hicho kinakwenda kinyume cha utamaduni wa Bunge.
“Kama ambavyo Serikali imeachwa ikasoma hotuba yake yote, msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni naye aachwe asome na aeleze kile ambacho ni maoni ya kambi, tangu kuanza kwa Bunge hili na mabunge yaliyopita, si utamaduni kukatisha hotuba ya upinzani,” alisema Lissu.
Lissu alisema wapinzani wamekuwa wakinyanyaswa na kwamba kuzuiwa kwa hotuba yao mara kadhaa, ni mbinu za kuwafanya wasieleze kwa Watanzania uovu unaofanywa na Serikali.
Baada ya hapo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisimama na kueleza kuwa anaunga mkono hoja ya Lukuvi kwa kuwa maelezo yaliyoko katika ukurasa wa nne wa hotuba ya upinzani yalitakiwa yakasemwe polisi.
“Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kwamba humu ndani ukurasa wa tatu kuna jambo ambalo jana (juzi) jioni ulitolea uamuzi kwa kutumia Kanuni ya 48 na nina imani kuwa waheshimiwa wabunge ambao wanajua hizi kanuni za kwenye vitabu watakubali kuwa hili jambo si la kujadili kwenye hotuba,” alisema Werema.
Alisema suala jingine ni la Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa na kwamba liko mahakamani na hata suala la Dk Steven Ulimboka nalo liko mahakamani.
“Naunga mkono hoja ya Waziri wa Nchi kwamba maneno haya yasiingie naomba kutoa hoja,” alisema Werema, huku akisema kuwa Lissu ni mtovu wa nidhamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment