WANASAYANSI
wa anga kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta uwezekano wa maisha katika
sayari nyingine, mbali na dunia.Kuna imani kuwa kwenye sayari hizo,
huenda zikapatikana raslimali nyingi kwa urahisi kuliko duniani ambako
binadamu wameishi mamilioni ya miaka hadi sasa.
Wataalamu hao wa
anga wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda sasa na moja ya mambo muhimu
wanayoangalia ni upatikanaji wa maji. Popote maji yanapopatikana,
wanaamini maisha yanawezekana.Moja ya sayari ambayo wamekuwa
wakiichunguza kwa miaka mingi sasa ni Mars, ambayo ni ya nne kutoka
kwenye jua. Dunia ni ya tatu.
Sababu kuu za kuichagua sayari hii tofauti na zingine ni kwamba, hali ya hewa inatofautiana kidogo sana na ya dunia.
Sayari
nyingine kama Mercury na Venus, zipo karibu zaidi na jua na hali ya
joto iko juu kiasi kwamba hali ya maisha inaweza kuwa taabu.
Mars
ambayo wanasayansi wanaipa jina la sayari nyekundu, ipo karibu na
dunia, hivyo ni rahisi kufika iwapo wanasayansi watathibitisha iwapo
maisha yanawezekana huko.
Wanaiita sayari nyekundu kwa sababu
eneo kubwa la uso wake ni wa rangi nyekundu, tofauti na nyingine
zilizomo kwenye mfumo wetu wa sayari.
Hakuna mwanasayansi ambaye
amethubutu kusafiri hadi kwenye sayari hiyo kutokana na ugumu wa kupata
vyombo vya kuaminika, vinavyoweza kusafirisha watu kutoka duniani hadi
Mars na kurudi salama.
Hata hivyo, hilo siyo tatizo kwa sababu wakibaini mazingira mazuri, utengenezaji wa vyombo hivyo hauwezi kuwapa taabu.
Kazi ya uchunguzi imekuwa ikifanywa kwa vyombo maalumu ambavyo havina watu lakini, vina uwezo wa kuleta mawasiliano duniani.
Pia
wanatumia viona mbali katika mchakato huo kuchunguza hali ilivyo
kwenye sayari hii, ambayo kumekuwapo na hisia kwamba huenda waliwahi
kuishi viumbe hai mamilioni ya miaka iliyopita lakini baadae mazingira
yakabadilika na kuwa mabaya.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, sayari
hii ina mabonde mengi ambayo yanakila dalili kuwa awali yalikuwa
yanatiririsha maji kama ilivyo mito hapa duniani.
Kwa muda mrefu, wanasayansi wamekuwa wakiichukulia sayari hiyo kuwa na mazingira ya jangwa yanayotokana na ukame wa muda mrefu.
Wagundua maji
Mwezi
uliopita wanasayansi hao wamekuja na maelezo kwamba sayari hiyo ina
kiwango kikubwa cha maji na mengi yapo mita chache kutoka uso wake.
Mmoja wa wanasayansi wanaochunguza sayari hiyo ni Profesa Jay Melosh wa Chuo Kikuu cha Purdue, nchini Marekani.
Yeye
anasema uchunguzi huo umewapa imani kwamba siyo tu kwamba Mars ina maji
bali kuna viumbe wadogo, mfano wa jamii ya bacteria ambao wanaendelea
kuishi humo hadi leo hii.
Ni uchunguzi ambao wanaamini una
matumaini tofauti na taarifa za uchunguzi uilizopita na kizuri zaidi pia
ni kubaini moja ya miezi yake miwili, maji yapo kwa wingi zaidi.
Miezi
inayoizunguka sayari ya Mars ni Demos na Phobos. Phobos ndio mwezi
uliogundulika kuwa na kiwango kikubwa cha maji na ndio ulio karibu zaidi
na sayari hiyo.
Kwa sababu hiyo, wanaamini kwamba maisha
yakianza kwenye sayari ya Mars, kuna uwezekano pia wengine wakahamia
kwenye mwezi huo wa Phobos.
Taarifa za uwepo wa maji kwenye
sayari hii zilitolewa kwenye mkutano wa wanasayansi wanaochunguza anga
za mbali, uliofanyika Austria Juni mwaka huu.
Moja ya dalili za uwepo wa maji ni vimondo ambavyo vimekuwa vikianguka kwa wingi kwenye uso wa sayari hiyo.
Mtaalamu
wa Uhandisi na Mambo ya Anga, Profesa Kathleen Howell anasema picha
walizopiga maeneo ambaye vimondo vimegonga uso wa Mars, zilionyesha
dalili kama za mtu aliyetupa jiwe kwenye eneo lenye tope.
No comments:
Post a Comment