Hili ndilo gari ambalo alilokuwa
akitumia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella
Mukangara, na kupata nalo ajali juzi akiwa safarini kutoka Dodoma
kuelekea jijini Mwanza kikazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Antony Luta, alithibitisha kutokea
kwa ajali hiyo majira ya saa 3:30 asubuhi katika Kata ya Nyandekwa
wilayani Igunga mkoani hapo, ikihusisha gari lenye namba za usajiri STK
8780.
Luta alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi la
Green Star lenye namba za usajili T939 TRA ambalo lilikuwa likitokea
Kahama kuelekea Dar es Salaam, alipokuwa akijaribu kulipita lori katika
mlima huku gari la Waziri huyo likitokea upande wa pili.
Dereva wa Waziri aliyetambulika kwa jina la Saidi Komando, alijaribu
kulikwepa basi hilo, lakini akashindwa na hivyo gari likapinduka mara
tatu na kusababisha watu watatu akiwemo Waziri Fenella, kujeruhiwa.
Kamanda Luta alisema mara baada ya ajali hiyo, Waziri huyo na majeruhi
wengine walikimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa matibabu
na kwamba mipango ya kuwahamishia katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
zinafanywa.
Dereva wa basi la Green Star, Daniel Chawa (32), alikamatwa baadaye na
polisi wilayani Igunga, baada ya kuwa amekimbia awali na hivyo
atafikishwa mahakamani.
Hali ya Dkt. Mukangara inaendelea vizuri.
Akiongea na Globu ya Jamii sasa hivi yupo Dar es salaam alikorejea jana
jioni na kupata matibabu zaidi katika kitengo cha mifupa cha MOI
hospitali ya Muhimbili. Amesema baada ya kuchukuliwa vipimo vyote,
ameonakana hana madhara mwilini zaidi ya michubuko na majeraha mengine
madogo. Anashukuru kwamba wote walikuwa wamefunga mikanda na kwamba
air-bags za gari hilo zimeokoa maisha yao.
Amewashukuru sana madaktari wa Nzega na wa kitengo cha dharura cha
Muhimbili ambao walimhudumia pamoja na wa hospitali ya Regency
alikopatiwa vipimo vya CT-Scan. Pia anawashukuru Watanzania wote
waliomuombea apate nafuu, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
No comments:
Post a Comment