Hakika kila chenye
mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa
jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya
muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa.
Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii, kuniamini na
kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia
chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni
heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha
maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku niliyoitumia katika Umoja
huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu.
Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na
watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa
katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.
Utumishi
wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa
pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani
niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na
madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia,
kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili
na udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine
nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za
pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake
katika kipindi cha mazingira magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto
za kipekee kabisa.
Daima
nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya
Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na
kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia
yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu
wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.
Hapana shaka
kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha kufahamiana kwa karibu
na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali mbali waliopata
mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya
michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi ya yote,
sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge waliokuwa
wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima tabasamu ya
mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani
Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa
na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa
amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini
alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa
amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.
No comments:
Post a Comment