Wachezaji wa Taifa stars wakiwa mazoezini
TIMU ya Taifa ya Tanzania, (Taifa Stars), leo ina kibarua 'kinene'
cha kusaka ushindi dhidi ya Ivory Coast watakaokuwa nyumbani kwenye
Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny, jijini Abidjan katika mchezo wa kwanza
kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka
2014.Mchezo wa leo unatarajia kuanza saa 11 jioni kwa saa za Ivory Coast
ikiwa ni saa mbili usiku kwa saa za Afrika mashariki.
Stars
iliyowasili Abidjan juzi jioni, inatazamia kupata kibarua kikali kutoka
kwa Ivory Coast iliyokusanya mastaa wake wote wakali wanaocheza soka la
kulipwa barani Ulaya wakiongozwa na Didier Drogba.
Stars ambayo
kocha wake, Kim Poulsen anajivunia zaidi mshambuliaji wa kimataifa
anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya TP mazembe, Mbwana Samata,
jana jioni ilifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya pambano hilo katika
uwanja Felix Houpheut Boigny.
Ingawa hakutaka kuweka wazi, lakini
kwa mujibu wa mazoezi ya jana, kocha Kim Poulsen anatazamiwa kufanya
mabadiliko mawili katika kikosi chake kilichotoka suluhu na Malawi Mei
26 katika Uwanja wa Taifa.
Bocco , Amir kuanza mechi:
Mlinzi Amir Maftaha anatarajia kuanza
upande wa kushoto akichukua nafasi ya Waziri Ally ambaye katika pambano
la kirafiki la kimataifa dhidi ya Malawi alionekana kuyumba kutokana na
kukosa uzoefu katika mechi za kimataifa.
John Bocco, ambaye ndiye
mchezaji mrefu zaidi katika kikosi cha Stars cha sasa anatazamiwa kuanza
katika safu ya ushambuliaji akiziba nafasi ya Haruna Moshi ‘Boban’
ambaye alianza katika pambano dhidi Malawi lakini ameachwa nyumbani kwa
kuwa majeruhi.
Hii ina maana Samata atacheza nyuma ya Bocco
atakayebaki mbele peke yake, tofauti na pambano lililopita ambapo Boban
alicheza nyuma ya Samatta.
Poulsen adai hana hofu:
Wakati homa
ya pambano hilo ikiendelee kuwanyemelea wachezaji wa Stars ambao
wamekuwa wakinyooshewa vidole vitatu na mashabiki wa Ivory Coast katika
mitaa wanayopita ikiwa ni ishara ya kufungwa mabao matatu, kocha Poulsen
amedai hana hofu kabisa na Ivory Coast na akawataka wachezaji wake
wafanye kazi iliyowaleta na kugeuza nyumbani wakiwa mashujaa.
“Sina
hofu na hata wachezaji wangu kama unavyowaona hawana hofu.
Tunawaheshimu Ivory Coast wana wachezaji wenye majina makubwa kama
Didier Drogba lakini nimewaambia wachezaji wangu waje kupambana na sio
kucheza na majina.”
Poulsen alisema kikosi chake kitacheza kwa
kadri kiwazavyo na hana mpango maalumu wa kuwadhibiti mchezaji mmoja
mmoja wa Ivory Coast.
“Tutacheza kwa nidhamu katika ulinzi na
tutakuwa tunaangalia namna ya kubadilika kadri mechi inavyokwenda.
Lakini mpango wa kumlinda mchezaji mmoja mmoja kama Drogba au Gervinho
hatuna. Tunahitaji nidhamu ya ulinzi wa pamoja,” alisema Poulsen.
Kwa
upande wa Ivory Coast, kocha wao Francois Zahoui ambaye ni staa wa
zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo aliyechukua nafasi ya kocha
maarufu, Sven-Goran Eriksson alisema anaihofia Stars kwa sababu
haifahamu vizuri.
“Sijawahi kuiona ikicheza kwa hiyo naihofia. Timu
nyingi ndogo zimekuwa zikicheza vizuri katika miaka ya karibuni.
Hatuwezi kuwadharau hata kidogo kwa sababu mpira wa siku hizi
umebadilika,” alisema Zahoui.
Timu hiyo itamkosa kiungo wa
Manchester City, Yaya Toure, pamoja na Emmanuel Eboue, Arthur Boka,
Cheik Tiote, Souleymane Bamba, na Didier “Maestro” Zokora walioamua
kupumzika kicheza timu ya taifa.
Tembo hao wanategemea kuziba nafasi hizo kwa kuwatumia chipukizi Marco Ne, Lacina Traore na Viera Diarrassouba.
Magazetini,
Ivory Coast wanaonekana wameshashinda mchezo huo dhidi ya Tanzania
ambayo haijawahi kufuzu kwa Kombe la Dunia hata mara moja.
Lakini mzozo wa sasa kuhusu uteteuzi wa kocha wa timu hiyo unaweza kuwa faida nyingine kwa Taifa Stars.
Mechi nyingine ya Kundi C itachezwa kaskazini mwa Afrika kwa Gambia kuikabili Morocco usiku huo.
No comments:
Post a Comment