Napenda nitahadharishe kuwa neno “mpya” mara nyingi huwa ni tata. Mtu anaweza kujiuliza ni upya wa nini: maudhui, muundo, jarada, mchakato, n.k? Je, ni kila kilichopo ndani ya katiba ya sasa kitatolewa?
Wakati mmoja Profesa Issa Shivji katika kitabu chake “Let the People Speak” aliwahi kusema kuwa katiba mpya tutakayokubaliana kutokana na mjadala wa kitaifa inaweza kurandana kwa kiasi kikubwa na katiba ya sasa kwa vifungu vyake ila kisiasa itakuwa ni kitu kipya kabisa kwa kuzingatia mchakato wenyewe uliotumika kupatikana katiba hiyo.
Professa alitoa angalizo hilo kwani mabadiliko ya katiba za huko nyuma hayakushirikisha watu wenyewe kufikia muafaka wa nini hasa wanakitaka. Badala yake CCM na serikali yake walitumia “top-down approach” kuhakikisha inawalinda kuhodhi madaraka.
Hili ni jambo la kimkakati kichama kwani hakuna chama chochote ambacho kinafurahia kutoka madarakani. Hivyo basi makala hii inaangalia kwa ukaribu ushiriki wa vyama vya siasa katika mchakato wa kutunga katiba.
Nianze kwa kusema kuwa vyama vya siasa ni taasisi muhimu katika demokrasia ya uwakilishi. Pamoja na kuwa na kazi nyingi kama vile kuelimisha, kushawishi watu kushiriki katika michakato ya kisiasa, kuandaa viongozi na hata kutunga sheria kupitia bunge, lengo kuu la chama chochote cha siasa huwa ni kushika dola.
Zipo njia mbalimbali za kutumiwa na chama kushika dola kama vile chaguzi za kidemokrasia, mapinduzi ya amani au mtutu wa bunduki. Kushika dola kupitia chaguzi kunahitaji utaratibu wa kisheria ambao msingi wake mkuu ni katiba ya nchi husika.
Pale chama kimoja kitaachiwa kuandaa taratibu hizi mara nyingi kitaziandaa kwa kujipendelea ili kuweza kushika dola na wakati huo kuweka mazingira magumu kwa wadau wengine kuking’oa madarakani.
Tofauti na lengo kuu la vyama vya siasa, katiba ni utaratibu mpana zaidi na inahusu nyanja mbalimbali za maisha husika ya wananchi kama vile umilikaji na mgao wa rasilimali za nchi, haki na wajibu wa raia, madaraka ya vyombo vya dola na masuala ya utamaduni.
Hivyo basi wakati lengo la kushika dola ni nyeti na pia hushughulikiwa na katiba pamoja na sheria husika, ifahamike kuwa kuitazama katiba kama nyenzo ya kufanikisha lengo hilo ni upungufu mkubwa.
Makala hii inajikita kuangalia nafasi ya vyama vya siasa katika mchakato wa kutunga katiba mpya kwa kuzingatia uzoefu wao na malengo ya vyama vyenyewe.
Hoja mahsusi ni kuwa ingawa vyama vya siasa ni wadau muhimu katika harakati za kutunga katiba mpya, ni hatari kuachia vyama hivyo kuwa nahodha wa kuratibu na kusimamia mchakato huo.
Makala itaonyesha uzoefu wa chama cha siasa katika kutunga katiba za 1962, 1964, 1965, na 1977. Pia itaonyesha hulka ya vyama vya siasa katika mchakato wa sasa wa kutunga katiba mpya. Itaibua nini tayari kimefanywa na vyama vya siasa na muelekeo wake kiujumla katika harakati za kupata katiba mpya.
Makala inashauri kuwa chama cha siasa kishiriki katika mchakato wa katiba mpya kwa usawa na wadau wengine ili kuweza kupanua maudhui ya katiba zaidi ya kushika dola tu.
Historia ya chama cha siasa kuchukua jukumu kuu katika mchakato wa kutunga katiba (au hata kufanya marekebisho ya vifungu/vipengele vyake) unaweza kujadiliwa kuanzia mwaka 1961.
Ikumbukwe kuwa Tanganyika (sasa Tanzania) ilijipatia uhuru wake mwaka huo toka kwa wakoloni wa Kiingereza kwa njia ya katiba iliyoruhusu “demokrasia” ya uwakilishi wa vyama.
Hivyo baada ya chaguzi za kabla ya uhuru, ni chama cha TANU ndicho kilishinda viti vyote, (isipokuwa kiti kimoja kilichochukuliwa na mgombea binafsi) na kushika dola.
Katiba hiyo iliruhusu pia vyama vya kiraia kama vile vyama vya wafanyakazi, wanawake, na vijana kufanya shughuli zao. Lakini kutokana na lile lengo kuu la chama cha siasa kushika dola, TANU ilianza kujipanga kukiritimba na kuhodhi madaraka ya nchi hususani kwa kuanzisha sheria mpya.
Kana kwamba hilo halikuweza kukidhi haja na matakwa ya ukiritimba huo, TANU ilianza mradi mkubwa wa kutunga katiba mpya. Sababu za kufanya hivyo zilitafutwa kila mara katiba mpya ilipotungwa. Hapo Tanzania ikajikuta ikitunga katiba mpya kama nne: Katiba ya Jamhuri (1962), Katiba ya Muungano (1964), Katiba ya Chama Kimoja (1965) na Katiba ya Kudumu (1977).
Katika kutekeleza azma yake ya kujihakikishia kutawala kwa muda mrefu, TANU ilianza kutumia mfumo wa sheria kudhoofisha aina yoyote ya upinzani. Kwa mfano, TANU ilifutilia mbali shirikisho la vyama vya wafanyakazi lililoitwa Tanganyika Federation of Labour (TFL) kwa kutunga sheria mpya National Union of Tanganyika Workers (Establishment) Act 1964. Sheria hii pia ilianzisha shirikisho jipya la wafanyakazi.
Athari bayana ya sheria hii ni pamoja na kuua uhuru wa vyama vya wafanyakazi nchini; na vyama vya wafanyakazi vilianza kuwekwa chini ya chama tawala na kufanya matawi ya TANU.
Hili lilifuatiwa na kufutwa kwa vyama vya siasa vya upinzani mwaka 1965 na kuanzisha mfumo wa siasa wa chama kimoja. Hapa katiba ya mwaka 1965 Ibara ya 3 ilitamka kuwa Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa chama kimoja na kuanisha kuwa TANU ndicho chama pekee kisheria Tanzania Bara na Afro-Shiraz Party (ASP) kiliendelea kuwa chama pekee huko Zanzibar. Hii ni kufuatia muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoundwa tarehe 26 Aprili 1964.
Zaidi sana matakwa ya mfumo wa chama kimoja yaliainisha kuwa masuala yote ya siasa mbali na yaliyohusu mihimili ya dola yaani bunge, mahakama na serikali yalifanywa chini ya chama tawala au moja kwa moja na chama chenyewe.
Kilele cha ukiritimba wa TANU kilifikiwa mwaka 1975 pale chama kiliposhika hatamu yaani chama kuwa ndicho chenye sauti na maamuzi ya mwisho katika kila jambo nchini.
Hapa serikali na mihimili yake ya dola ilitiwa mfukoni mwa chama tawala. Ilikuwa vigumu kutenganisha chama na serikali. Huo ulikuwa ndiyo mwanzo wa “chama dola” kutokea hapa nchini.
Ingawa matukio yaliyotajwa hapo juu yaliashiria kuwepo mfumo wa chama kimoja kisheria, wanazuoni wengi wanakubaliana kuwa mfumo huo ulikuwepo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1962.
Mambo matatu yanaweza kuonekana katika michakato ya kutunga katiba mpya zilizopita au kwa kufanya marekebisho ya katiba hizo kama ifuatavyo: Mosi, ni kwa kutumia mfumo wa sheria chama tawala kimejihakikishia kushika dola kwa muda mrefu.
Ifahamike kuwa chama tawala ndicho kilihusika moja kwa moja kutunga katiba kwaniaba ya wananchi. Serikali ilikuwa ikitekeleza tu maagizo ya chama. Pili wananchi walipokonywa haki yao ya kuhusika kutunga katiba mpya na hivyo katiba kutafsiriwa kama “mkataba kati ya watawala na watawaliwa” kinyume cha tafsiri ya sasa kuwa “katiba ni muafaka wa kitaifa.” Tatu ni ukweli kwamba katiba imeendelea kupoteza uhalali wa kisiasa.
Kuelekea mageuzi ya mfumo wa kisiasa toka chama kimoja kwenda demokrasia ya vyama vingi, suala la katiba mpya lilipendekezwa na tume ya Rais, maarufu kama Tume ya Nyalali.
Hata hivyo CCM ilipuuza mapendekezo ya kutunga katiba mpya. Licha ya utetezi mbalimbali kutolewa na chama tawala na serikali yake kukataa kutunga katiba mpya, ukweli unabaki kuwa hofu ya CCM kung’olewa madarakani imeendelea kuwa tatizo.
Waasisi wa CCM, hususani Pius Msekwa, wanadai kuwa ili hoja ya katiba mpya iweze kuwa na mantiki ni lazima walau jambo moja litokee kati ya haya: mabadiliko ya dola; kuunganika kwa dola; katiba iliyokuwepo kufutwa na dikteta; pale demokrasia inapoangusha utawala wa kibaguzi; na yanapotokea mazingira maalum.
Itaendelea wiki ijayo
No comments:
Post a Comment