..

..
.

Friday, 22 June 2012

Mbowe, Lissu, Mdee wamzima Ngeleja



MAKEKE ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (CCM), jana yalizimwa na wabunge watatu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Halima Mdee, huku wakimtaka Spika wa Bunge amchukulie hatua kwa kupoteza muda.
Ngeleja aliyekuwa akichangia hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 muda mfupi baada ya Mbowe, alitumia muda mwingi kuishambulia hotuba ya maoni ya bajeti ya Kambi ya Upinzani akidai ni mbovu na haitekelezeki.
Huku akishangiliwa na wabunge wenzake wa CCM, Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, alikwenda mbali zaidi akinuku hotuba hiyo iliyowasilishwa na Waziri kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, na kusema kuwa wana vyanzo vya ukusanyaji mapato ambavyo vinaonesha shilingi sifuri.
Kama hiyo haitoshi, mbunge huyo aliitaka Kambi ya Upinzani kuwaomba radhi Watanzania akidai wamewapotosha kutokana na kuandaa bajeti iliyowahadaa wakati wameshindwa kuainisha uwiano wa vyanzo vya mapato na matumizi.
Hatua hiyo, ilimfanya mnadhimu mkuu wa kambi hiyo, Lissu kusimama na kuomba mwongozo wa Spika akisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, bajeti iliyoko mbele yao ambayo inapaswa kujadiliwa ni ile iliyowasilishwa na serikali.
“Sisi wapinzani tunawasilisha maoni yetu kuhusu bajeti ya serikali ili yafanyiwe kazi na si bajeti kivuli wala mbadala kama baadhi ya wabunge wanavyojaribu kupotosha,” alisema Lissu na kuungwa mkono na Spika.
Spika Anne Makinda alifafanua kuwa hakuna bajeti kivuli wala mbadala na badala yake kambi hiyo hutoa hoja ya kuhusu bajeti ya serikali inayokuwa imesomwa ikionesha kama wao wangekuwa madarakani wangeipanga hivyo.
Hata hivyo Ngeleja aliikataa taarifa hiyo na hivyo kuzidi kushikilia msimamo wake, jambo lililomlazimu Mbowe, kuomba mwongo wa Spika akiuliza kiti chake kinawachukulia hatua gani wabunge kama hao wanaopoteza muda kwa jambo lililokwisha kufafanuliwa.
Wakati Spika akijaribu kumaliza ubishi huo, Mbunge wa Kawe, Mdee, aliinuka na kuomba kumpa taarifa Ngeleja na kusema kuwa kipengele anachokisemea mbunge mwenzake kilishatolewa ufafanuzi kwamba kulikuwa na kasoro za uchapaji.
“Huyu ana uchungu wa kutemwa katika Baraza la Mawaziri,” alisema Mdee lakini kabla ya kuendelea Spika alimtaka afute maneno hayo kwanza.
Mdee alidai kuwa hatua hiyo inaonesha ni jinsi gani Ngeleja haudhurii vikao, kwani asingepoteza muda kuhoji jambo ambalo walikwisha kulifanyia masahihisho.
Awali wakati wa mchango wake, Ngeleja alisema kuwa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa sasa inachangiwa na upungufu wa chakula ambapo bei ya bidhaa hiyo imepaa na kuongeza makali ya maisha kwa wananchi.
Ngeleja alisema pia tatizo la nishati limekuwa chanzo cha kuongeza makali ya maisha kwani bei ya nishati imekuwa ikipaa mara kwa mara.
Naye Mbowe katika mchango wake, mbali na kulalamikia deni la taifa na kuitaka serikali ifanye juhudi za makusudi kuwaondoa wananchi kwenye umaskini walionao sasa, pia alikemea lugha za matusi kwa baadhi ya wabunge, hivyo kumtaka spika na wasaidizi wake kutenda haki kwa pande zote.
Shellukindo awasifu wapinzani
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo, (CCM), alianza kwa kuipongeza kambi ya upinzani bungeni akisema kuwa inafanya kazi yake vizuri kwa kuishauri na kuikosoa serikali.
Shellukindo aliwataka wabunge wenzake wa chama tawala kuweka mambo ya vyama pembeni na kuangalia masilahi ya taifa, kwani kazi ya wabunge wote bila kujali itikadi za vyama ni kuishauri serikali katika masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema hakuna Bunge katika nchi yoyote ambalo ni la chama tawala wala cha upinzani, huku akiwapongeza wapinzani kuwa wanakitakia mema CCM kwa kuwakosoa ili warekebishe.
Aidha, mbunge huyo alikosoa sera ya Kilimo Kwanza huku akibainisha kuwa haimlengi mkulima wa kawaida bali ni wakulima wakubwa.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Selukamba (CCM), alisema mfumuko wa bei unachangiwa na ubovu wa miundombinu jambo ambalo husababisha mazao yanayotoka shambani ambako ni vijijini kufika mjini na kuwa katika bei ya juu kuliko yalivyozalishwa.
Selukamba alibainisha kuwa mazao au bidhaa ikitoka kijijini inapofika mjini huuzwa kwa bei ya juu zaidi kutokana na gharama kubwa kutumika katika usafirishaji wake.
Filikunjombe aigomea bajeti
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), naye amekuwa kama mwenzake wa Kisesa, Luhaga Mpina, kwa kugoma kuiunga mkono bajeti ya serikali akitaka maelezo ya serikali kuhusu fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa katika Wizara ya Uchukuzi.
“Katika bajeti iliyopita tulisema na serikali kupitia waziri mkuu, ikatangaza kuongeza sh bilioni 90 kwa Wizara ya Uchukuzi na kati ya hizo sh bilioni sita, zilipelekwa katika sekta ya meli Ziwa Nyasa na fedha zilizoletwa ni sh milioni 200 pekee,” alisema.
“Nawaomba wabunge wenzangu tuwe wakweli, kwa hili  lazima tuihoji, na kwa serikali hii ya CCM ni yetu, kama hatutafanya hivyo tutakuwa hatuna maana ya kuwapo kwetu hapa bungeni,” alisema Filikunjombe.
Mkono aibua ufisadi
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, ameibua ufisadi unaodaiwa kufanywa katika mgodi wa Kiwira na kulitaka Bunge kuunda kamati maalumu ya uchunguzi.
Mkono alidai kuwa sehemu moja ya mgodi huo yenye utajiri mkubwa imeuzwa kwa bei ya kutupwa kwa kampuni moja ya Australia.
Alisema uuzaji huo ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa na Bunge  mwaka 2007 ambapo liliagiza kuwa mgodi wa Kiwira uliokuwa umeuzwa kwa Kampuni ya Tan Power urudishwe serikalini baada ya kuwa umeuzwa kwa dola laki saba tu.
Hata hivyo, Mkono alisema kuwa katika hali ya kushangaza Kampuni ya Tan Power ambayo ilikuwa imeingia ubia na serikali iliuzwa kwa Waustralia  kiasi cha mabilioni ya dola.
“Mheshimiwa Spika, Kiwira kulikoni? Lini Bunge litaunda kamati ya kwenda kuangalia Kiwira?” alihoji na kusema kuwa pamoja na yote hayo, sasa serikali imetenga sh bilioni 40 kwa ajili ya mradi wa Kiwira na kuhoji nani aliteketeza fedha za awali zilizotolewa kwa ajili hiyo.

No comments:

Post a Comment

KARIBU