Bajeti
ya Serikali imepita huku wabunge wa upinzani wakiipinga na baadhi ya
wabunge wa CCM wakionyesha msimamo wa kuikataa tangu awali na wengine
wakiingia mitini muda mfupi kabla kura kupigwa.
Luhaga Mpina (CCM), ambaye alionyesha kuikataa bajeti hiyo tangu awali
alitoka muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji kura kwa kuitwa majina
mmoja baada ya mwingine.
Kabla ya kutoka nje, Mpina alionekana akijadiliana jambo na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) na baada ya hapo
hakurejea tena kwenye kiti chake.
Mwingine aliyepinga bejeti hiyo katika michango yao lakini hakuwepo
wakati wa upigaji wa kura ni Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM)
pamoja na Kangi Lugola (CCM, Mwibara).
Mbunge pekee wa upinzani aliyepiga kura ya ndio kuikubali bajeti hiyo
ni John Cheyo, wa Baridi Mashariki (UDP), wakati Mbunge wa Kuteuliwa,
James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alipinga bajeti hiyo kwa kusema hapana.
Uchunguzi wa mtandao huu, umebaini kuwa kulikuwa na mawasiliano baina
ya Mpina na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na
Uratibu, Steven Wassira.
Mawaziri hao walionekana wakiwa wamekaa na Mpina kwenye viti viwili
pamoja ambavyo vimewekwa kwenye lango kuu linalotumiwa na maofisa wa
serikali na waandishi wa habari.
Hata hivyo, Waziri Wassira alianza kuzungumza nae kwa kile kilichoelezwa kuwa akubali kuiunga mkono bajeti hiyo.
Mpina alipotafutwa kuzungumzia hatua yake ya kutopiga kura alisema,
Lukuvi alimwendea na kumweleza kuwa kwa sababu Muswada wa Sheria ya
Fedha utajadiliwa baada ya bajeti kumalizika kuna nafasi ya kuzitafuta
fedha hizo kwenye bajeti za wizara.
Alisema pamoja na maelezo ya Waziri Lukuvi alishindwa kuingia na kupiga
kura kwa maelezo kuwa Dk. Mgimwa wakati akihitimisha hotuba ya bajeti
hakujibu hoja zake kama alivyoelezwa na Lukuvi.
Alisema bado kuna nafasi nyingine ambapo atatoa hoja zake kwenye bajeti
za wizara zinazofuata na mwishowe kwenye huo Muswada wa Sheria ya
Fedha.
“Sikuweza kupiga kura kwa sababu sikuelewa kama hoja zangu kweli
zimezingatiwa…maana yake niseme “ndiyo” kwa nini na nisema “hapana” kwa
nini wakati hoja zangu hazijajibiwa,” alisema.
Wabunge walionekana kupiga makofi wakati majina ya wabunge ambao awali
walionyesha msimamo wa kupinga bajeti hiyo walipopiga kura za ndiyo au
hapana.
Mapema siku moja kabla ya kupitisha bajeti hiyo, juzi usiku, baadhi ya
mawaziri na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walikesha kwa ajili ya kupanga
mikakati ya kuweza kupangua hoja zilizotolewa na wabunge kuhusiana na
bajeti hiyo.
Chanzo cha habari hizi kimesema kuwa kikao hicho ambacho kilianza saa
3.30 usiku na kumalizika saa 9.30 alfajiri, kilifanyika chini ya Waziri
Mkuu Pinda.
Uchunguzi wa mtandao huu, umebaini kuwa kikao hicho kilifanyika nyumbani kwa Waziri Mkuu eneo la Uzunguni mjini hapa.
Baadhi ya mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Dk. Mgimwa, Wassira, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu na Waziri
Lukuvi.
Idadi ya kura zilizopigwa na kusema ndiyo ni 225 na kura 72 zilisema hapana wakati wabunge 54 hawakuwepo.
Mapema akitoa majumuisho ya michango ya wabunge kuhusu bajeti ya
serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Mgimwa, alisema Serikali
imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa viwanda vya nguo,
lakini haikupunguza kodi ya pato la mishahara kwa (PAYE) inayotozwa kwa
wafanyakazi.
Kadhalika, alitangaza kuanzia mwaka huu wa fedha wafanyabiashara
wanaopata faida ya shilingi milioni tatu kwa mwaka hawatalipa kodi ya
mapato badala yake kodi hiyo itaanza kutozwa kwa wafanyabiashara
wanaopata faida inayoanzia shilingi milioni nne kwa mwaka.
Kwa mujibu wa maelezo hayo wafanyabiashara wa ‘boda boda’ wamefutiwa kodi ya mapato.
Aidha alisema serikali imekubali kuondoa VAT kwa viwanda vya mafuta
ya kula lakini pendekezo hilo litawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri wa
Afrika Mashariki kwa maamuzi zaidi na maelekezo yake yataletwa wakati
wa mjadala wa muswada wa fedha.
Kadhalika alisema serikali haitaweza kuongeza kima cha mshahara
kufikia Sh. 315,000 kwa mwezi kwani kutaongeza bajeti ya uendeshaji
kwa kiasi cha Shilingi trilioni sita.
Akijibu hoja ya wabunge kutaka kujua maeneo yaliyosababisha deni la
taifa kukua kutoka trilioni 5 mwaka 2009 hadi kufikia trilioni 20 mwaka
wa fedha wa 2012/13 alisema, miradi iliyosababisha deni hilo kukua ni
pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Mkula hadi Kigoma.
Nyingine ni barabara za Dar es Salaam – Somanga, na Shelui -Nzega, Singida –Babati—Minjingu.
Pia mradi wa umeme wa Songosongo, Kihansi, mradi wa umeme wa Nyakato
na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na ukarabati na ujenzi wa
viwanja vya ndege vya Songwe na Mwanza.
Jumla ya Sh. trilioni 15, zilipitishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na kuendesha shughuli za serikali kwa mwaka 2012/13.
No comments:
Post a Comment