MAMLAKA ya maji safi na maji taka Jijini Arusha(AUWSA ),imebaini kuhujumiwa wa watu mbalimbali wakishirikiana na wafanyakazi wake, wasio waaminifu kwa kuunganisha maji kinyume cha utaratibu na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa AUWSA, Eng.Ruth Koya alisema jana kuwa, tayari
wamefanikiwa kuwanasa wezi wa maji zaidi ya 100 waliojiunganishia
kinyume na utaratibu, wakiwemo vigogo wa halimashauri ya Arusha,ambao
wamekuwa wakitumia huduma hiyo kwa kipindi kirefu,bila kulipa chochote
na kuisababishia hasara kubwa mamlaka hiyo.
Vigogo
wa halmashauri waliokamatwa ni pamoja na Afisa mali asili, mazingira
na ardhi, Maico Myairwa ambaye yeye aling’oa kabisa mita ya idara ya
maji, ambayo imekutwa chumbani mwake, ameificha huku akijua ni kosa
kisheria.
Mwingine
ni fundi mkuu wa maji wa halmashauri ya Arusha,Loishono Mollel ambaye
amejiunganishia maji baada ya kutoboa bomba kubwa la idara ya maji na
kupitisha mpira mrefu kwa chini, hadi nyumbani kwake ambapo pia
alikuwa akiyatumia maji hayo kustawisha bustani yake.
Hata
hivyo Mollel amebainika kuwa kinara mwenye mradi wa kuwaunganishia
maji watu mbalimbali kinyemela, huku wakimlipa kiasi kikubwa cha fedha
,ambapo mamlaka hiyo imengóa mtandao wa mabomba yote aliyoyaunganisha
kwa wakazi mbalimbali eneo la Sekei na kufanya familia zaidi ya 20,
kukumbwa na adha ya kukosa maji.
Pia
meneja wa maji wa halmashauri ya Arusha, Criston Kimaro ambaye ndiye
anadaiwa kutoa idhini ya watu kuunganishiwa maji bila kufuata utaratibu
huku watu hao wakimlipa fedha ya kuwaunganishia pamoja na malipo ya
mwezi katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Operesheni
hiyo ikiongozwa na mkurugenzi wa maji safi na maji taka wa jiji la
Arusha ,Engineer Koya na kuambatana na maafisa wengine ,imekuja
kufuatia kuwepo taarifa za upotevu mkubwa wa maji, tofauti na kiwango
kinachozalishwa kwa siku na kufanya idadi kubwa ya wateja wake, kutopata
huduma ya maji safi baada ya nusu ya maji yanayozalishwa, kuishia
njiani kwa wajanja wachache.
Eng,Koya
alisema maji yanayozalishwa na AUWSA ni mengi kutoka katika vyanzo
vyake mbalimbali, lakini amekuwa akishangazwa kupata malalamiko ya kila
mara kutoka kwa wateja wake wa kudumu na wapya kwamba hawapati huduma
hiyo.
Alisema
Operesheni hiyo ni yakudumu lengo ni kuhakikisha wanaondoa mtandao wa
wezi wa maji, ambao wamekuwa wakijinufaisha bila kuilipa chochote
mamlaka hiyo,na kwamba watawafikisha mahakamani watu wote waliohusika
na wizi huo wa maji iwapo watashindwa kulipa fidia katika kiwango
walichotumia .
Naye
mkuu wa kikosi cha operesheni wa AUWSA,Mohamed Isumail alisema, tangu
kuanza kwa zoezi hilo,Mei 29 mwaka huu watu zaidi ya 100 kutoka maeneo
ya Moshono,Sekei,Lemara na Ungalimited wamekamatwa, baada ya kubaini
wamejiunganishia huduma ya maji na kutumia kinyume na utaratibu .
Aidha
alisema maeneo yaliyokithiri kwa wizi wa maji jijini hapa ni
,Sekei,Moshono Migungani na Baraa, ambapo idadi kubwa ya wakazi wa
maeneo hayo, wanaiba maji baada ya kuunganisha mipira mirefu chini ya
Ardhi huku wakiwahadhaa waofisa wa maji waporika, kuwa maji wanayotumia
yanatoka kwenye bomba la kijiji ambayo mara nyingi hayalipiwi.
Isumaili
ambaye pia ni kaimu Mhandisi,uendeshaji na matengenezo AUWSA,aliongeza
kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika zoezi hilo, ni pamoja na watu
kujifungia ndani na kugoma kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment