Mgomo
wa madaktari umeanza tena, siku chache zilizopita. Inasikitisha kuona
kuwa tumefikia hali hiyo. Ukiniuliza nani namhesabu kama mwajibikaji
mkuu aliyesababisha tatio hili, nitakuambia kuwa ni serikali ya CCM. Huo
umekuwa msimamo wangu tangu pale ulipotokea mgomo wa mwanzo wa
madaktari wiki kadha zilizopita. Nilieleza msimamo huo hapa.
Siku chache zilizopita, nilimsikiliza mwenyekiti wa madaktari
wanaogoma, Dr.Stephen Ulimboka, akiongelea jinsi uhaba wa vitendea kazi
ulivyo. Alitaja mfano wa kifaa cha "CT-scan" ambacho kimeharibika
Muhimbili yapata miezi mingi iliyopita.
Kama nilivyosema katika makala yangu ya mwanzo, sera za serikali ya CCM
zinasabisha upotevu mkubwa wa mali ya Tanzania, kama vile madini.
Serikali yenyewe imekiri kuwa mikataba ya madini ya siku zilizopita
ilikuwa ni ya hasara kwa Taifa. Lakini je, serikali imeshamwajibisha
yeyote aliyehusika katika kusaini mikataba hiyo?
Je, ni kweli kuwa nchi hii haiwezi kununua hicho kifaa cha "CT-scan"?
Kutokana na sera mbovu za CCM, makampuni kama Barrick yanafaidika sana
na dhahabu yetu wakati sisi, ukifananisha na mapato wanayopata wao, sana
sana tunaambulia mapato duni sawa na njugu kiganjani, na tunaambulia
uharibifu wa mazingira na afya za watu wanaoishi maeneo ya migodini,
Kitu kimoja kinachokera katika mgogoro huu baina ya serikali na
madaktari ni jinsi madai ya madaktari yanavyopotoshwa. Wako ambao
wanaongea kama vile wanachodai madaktari ni posho na maslahi yao tu.
Ukweli ni kuwa madaktari wana madai ya msingi ya kuwatetea wananchi.
Kuna uchakachuaji wa makusudi unaofanywa kuhusu jambo hilo, ili
ionekane kuwa madaktari hawajali maishai ya wananchi.
Ni kweli kuwa mgomo huu unaathiri maisha ya wa-Tanzania. Hili si jambo
jema. Lakini serikali haina haki ya kuwashutumu madaktari kwa hoja hii
ya kutojali maisha ya wa-Tanzania, wakati serikali hiii hiii
inawakumbatia hao wanaoitwa wawekezaji ambao wengi wao wanahujumu maisha
na afya za wa-Tanzania, achilia mbali kuharibu mazingira maeneo ya
migodini. Serikali ingekuwa haifanyi hayo, ingekuwa na haki ya
kuwaandama madaktari kwa hoja hii ya kuathiri maisha ya wa-Tanzania.
Katika mgogoro baina ya serikali na madaktari, kuna pia suala la
serikali kutumia mwanya wa sheria na uamuzi wa mahakama. Serikali
haifanyi haki inapokwepa kuwajibika kwa yale yanayodaiwa na madaktari,
madai ambayo ni ya kweli, na yako katika uwezo wa serikali na nchi yetu
hii ambayo ina utajiri mkubwa. Kama suala ni sheria na maamuzi ya
mahakama, sote tunakubali kuwa sheria ichukue mkondo wake.
Lakini kinachokera ni kuwa serikali inatumia mwanya huu kufunika kile
ambacho sisi wengine tunakiona ni uzembe na kutowajibika kwa serikali
yenyewe. Madai ya madaktari ni ya msingi, na yako katika uwezo wa
serikali hii. Kwa serikali kutowajibika hapo na kukimbilia mahakamani
kuwabana madaktari kwa kipengele cha sheria tu, sio jambo la haki na
haliiweki serikali katika sura nzuri, kwa mtazamo wangu.
Kama nilivyosema katika makala yangu ya mwanzo, kugombana na madaktari
si jambo jema. Nilikumbushia usemi wa wahenga kuwa tusidharau wakunga
na uzazi ungalipo. Napenda kuongezea kwa dhati kabisa kuwa kugombana na
madaktari si dalili njema bali ni uchuro.
No comments:
Post a Comment