Milolongo isiyomalizika ya watu waliojaa huzuni na fahari wanaendelea
kupita mbele ya jeneza lililofunikwa nusu, la shujaa wao wa taifa Nelson
Mandela na kumpa hishma zao za mwisho .
Jeneza la Nelson Mandela limewekwa katika ukumbi wa Union Buildings
Milolongo isiyomalizika ya watu waliojaa huzuni na fahari wanaendelea
kwa siku ya tatu Umati wa watu wanapiga foleni tangu alfajiri huko
Pretoria wakitaraji kumpa hishma za mwisho shujaa wao Nelson Mandela
kabla ya maiti yake kusafirishwa hadi katika kijiji alikozaliwa ambako
ndiko atakakozikwa jumapili ijayo.
"Kumuona kwa mara ya mwisho,ni jambo linalonituliza moyo" anasema Tieho
Motspal,anaepiga foleni pamoja na mkewe tangu saa sabaa za usiku wa jana
kuamkia leo.
"Tutakapomuona rais wetu tu,tutarejea nyumbani,katika mji mdogo wa
Frankfurt, saa tatu kwa gari kutoka Pretoria, anasema Tieho Motspal
akizungukwa na maelfu ya wengine, wanaosubiri kupita mbele ya jeneza la
shujaa wao.
Jana jioni maafisa wa serikali waliifunga milango ya ikulu-Union
Buildings,ambako maiti ya Nelson Mandela imewekwa,katika wakati ambapo
maelfu walikuwa bado wamepiga foleni kusubiri kuingia.
Baadhi ikiwa ni pamoja na Stanley Luvhimbe aliyesafiri masafa ya
kilomita 450 hadi Pretoria wakaamua kulala nje kususbiri hadi leo:"Ni
fursa pekee.-hatutomuona tena" anasema.
Leo ni Siku ya Mwisho
Waafrika kusini bila ya kujali kabila wala dini wanamlilia shujaa wao
Wengine wamekuja leo kubahatisha kama watafanikiwa
kumuona,mfano wa Ompelege Majafa mwenye umri wa miaka 27 aliyesafiri kwa
muda wa saa tatu usiku kucha."Ni tukio ambalo kamwe hatutolisahau"
anasema.
Kila asubuhi na kwa muda wa siku tatu sasa,maiti ya bingwa wa mapambano
dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid ,rais wa kwanza
mweusi wa Afrika kusini,inatolewa katika hospitali ya kijeshi ya
Pretoria na kuletwa katika ikulu ya Union Buildings.
Jeneza lake likiwa ndani ya gari na kufuatiwa na mlolongo wa magari
mengine na pikipiki za serikali huzunguka barabara za mji mkuu ambako
wananchi wanasimama njiani wakipepea bendera kumpa hishma na kumuwaga
baba wa taifa.
"Watu wana huzuni lakini siamini mie kama wanahisi mustakbal wao
hautakuwa mwema.Nnahisi tuna mengi ya maana yanayotufanya tuamini
tutakuwa na mustakbal mwema.Na hata kama tumempoteza mbabe shujaa
wetu,naamini kuna mambo mengi mazuri yanayotoa matumaini mema. Afrika ya
Kusini tumejifunza na tunajifunza kutoka kwa Nelson Mandela na kila
mmoja anajiuliza atachangia vipi kuyafanya mambo yawe bora."
Maiti ya Nelson Mandela itasafirishwa kwa ndege kesho alfajiri hadi
katika kijiji alikozaliwa cha Qunu alikousia mwenyewe ndiko anakotaka
akazikwe.
Kamera na Wageni Hawatoruhusiwa
Kansela Angela Merkel aandika katika daftari la rambi rambi katika ubalozi wa Afrika kusini mjini Berlin
Mazishi rasmi ya jumapili yatahudhuriwa na watu kama elfu tano
hivi wakiwemo pia viongozi mashuhuri wa kimataifa ikiwa ni pamoja na
mwanamfalme Charles wa Uingereza.
"Kamera hazitaruhusiwa wakati wa mazishi, familia haitaki watu waone
maiti itakapoteremshwa kaburini," amesema msemaji wa serikali Phumla
William. Vyombo vya habari na wageni wa hishma hawatoweza kuhudhuria,
amesisitiza.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/
Mhariri: Mohammed Khelef
No comments:
Post a Comment