..

..
.

Saturday, 20 July 2013

Koo zinazopigana Kenya zatoa wito wa kusimamisha vita kwa ajili ya Ramadhani

Mapigano baina ya koo zenye uhasama za Degodia na Gare kaskazini mashariki ya Kenya yamesimama kwa kuwa viongozi wao walikubaliana kuleta amani wakati wa Ramadhani na kuahidi kuendelea kulifanyia kazi pamoja kuelekea amani hata baada ya mwezi mtukufu wa Kiislamu.
Kiongozi wa jamii ya Gare Sultan Yussuf Ibrahim (kulia) na mwenzake ambaye hakutambulika wa Degodia wakipeana mikono tarehe 4 Julai kama ishara ya kumaliza uadui baina ya jamii zao mbili. [Na Bosire Boniface/Sabahi]
Waislamu wa Garissa wakijitayarisha kushiriki kwa futari, chakula ambacho hufungua mfungo wa kila siku ifikapo jua kutua wakati wa Ramadhani. Wakaazi wa kaskazini mashariki ya Kenya wanautumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kutangaza amani na maelewano. [Na Bosire Boniface/Sabahi]
  • Kiongozi wa jamii ya Gare Sultan Yussuf Ibrahim (kulia) na mwenzake ambaye hakutambulika wa Degodia wakipeana mikono tarehe 4 Julai kama ishara ya kumaliza uadui baina ya jamii zao mbili. [Na Bosire Boniface/Sabahi]
  • Waislamu wa Garissa wakijitayarisha kushiriki kwa futari, chakula ambacho hufungua mfungo wa kila siku ifikapo jua kutua wakati wa Ramadhani. Wakaazi wa kaskazini mashariki ya Kenya wanautumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kutangaza amani na maelewano. [Na Bosire Boniface/Sabahi]
Waislamu na Wakristo wa Kenya watangaza amani wakati wa Ramadhani
Wiki kadhaa za mapambano baina ya koo yaliua angalau watu 50 na kuwasambaratisha wengine wengi, lakini mkaazi wa Kaunti ya Mandera kutoka ukoo wa Gare Omar Ali Kerrow mwenye umri wa miaka 33, alikaribisha hatua hiyo ya maridhiano.
"Tangu Ramadhani kuanza tarehe 10 Julai, uadui tuliokuwa nao baina yetu umeshuka chini," alisema kerrow, anayeishi katika wilaya ya Rhamu. "Tunatarajia kuendelea na amani hata baada ya Ramadhani."
Tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Kerrow alisema ameifanya kuwa ni sehemu ya kukaribisha na kushiriki au kujiunga na rafiki kutoka ukoo wa Degodia) kwa ajili ya futari, chakula kinachoashiria mwisho wa kufunga katika siku.
"Huu ni mwezi ambao tunapaswa kuimarisha kuwepo kuishi pamoja kwa amani kwa sababu sisi ni Waislamu wote na hakuna haja ya kupambana baina yetu," aliiambia Sabahi.
Duka la bidhaa mchanganyiko la Kerrow lilichomwa moto wakati wa mapigano baina ya koo, lakini alisema kuwa hana hisia mbaya kwa waliomtendea maovu. "Ili kuendelea mbele, mimi nimeomba msamaha kwa wale niliowafanyia mabaya niliyotenda wakati wa mapigano. Pia nimewasamehe wale walionikosea," alisema.
Mkaazi wa Rhamu Mohammed Mursal Amin mwenye umri wa miaka 30, alisema kuwa baada ya miezi ya wasiwasi, hatimaye Ramadhani imeleta amani katika eneo hili.
"Tunafanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa halitarejea," Amin aliiambia Sabahi. "Ikiwa ungeniuliza ninatoka ukoo gani wakati ule wa mapambano, ningekuambia kwa kujidai kabisa kuwa mimi ni wa kutoka Degodia, lakini sasa mimi ni Muislamu. Nitabakia kuwa hivyo hata baada ya Ramadhani. Waislamu hawapaswi kupigana wenyewe kwa wenyewe kwa jina la ukoo wao."

Zawadi ya Ramadhani

Amin alisema kuwa alipoteza jamaa zake watatu na duka lake wakati wa mapigano, lakini ameona kuboreka kwa amani tangu amani iliposainiwa baina ya koo zinazopigana tarehe 4 Julai -- na kujulikana kama "zawadi ya Ramadhani".
Familia nyingi zilizosambaratika kwa mapigano ziliweza kurejea majumbani mwao kwa kuwahi mwezi wa Ramadhani, alisema. "Tunafanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kuwa makubaliano ya amani yanadumu muda mrefu zaidi baada ya Ramadhani," Amin alisema.
Hadi sasa, wakaazi wameitikia wito wa amani na hakujakuweko na tukio la vurugu baina ya makabila tangu walipokubali mkataba huo wa amani, alisema.
Viongozi katika Msikiti wa Rowla kwenye mji wa Mandera wamewataka wakaazi kuchanganyika na kugawana vyakula vyengine kama vile daku, chakula kinachoashiria kuanza kwa kufunga, alisema Imam Sheikh Yusuf Ali.
"Huu ni mwezi ambao tunahamasisha walio waaminifu kuzungumza baina yao na kutakana msamaha," aliiambia Sabahi. "Ramadhani ilikuja wakati muafaka kabisa. Pia kuna suala la uadui unaochemka baina ya Waislamu na Wakristo kuhusu mashambulizi ya ugaidi. Ni mwezi muafaka wa kuonyesha jinsi Uislamu ulivyo kuhusu amani."
Ingawaje kuna Wakristo wachache huko Mandera, Waislamu wametakiwa kuwakaribisha majirani zao ambao sio Waislamu kushiriki katika futari, Ali alisema.
Katika Msikiti wa Nur mjini Mandera, waumini wanaomba amani miongoni mwa jamii katika kaunti na nchi, alisema Imam Sheikh Mukhtar Abdi.
"Tunamuomba Mungu atuunganishe tena ... asimruhusu shetani kutugawa. Tumemuomba Mungu kuifanya Ramadhani hii kuwa mahali pa kuanzia umoja wetu," aliiambia Sabahi.
"Ninatiwa moyo na kukumbatiana, tabasamu na mwangwi wa vicheko vya moyo miongoni mwa waumini ambao awali walikuwa hawatazamani machoni na waliokuwa wakiwajua kama maadui hapo zamani," alisema.

Kushajiisha amani kati ya koo na dini

Gavana wa Kaunti ya Wajir, Ahmed Abdullahi, aliiambia Sabahi kwamba hatua kama hizo za kufuturu pamoja mwezi wa Ramadhani zilikuwa zinafanyika hapo.
"Mapigano ya Mandera yalisambaa hadi Wajir, yakisababisha vifo vya watu watano," alisema. "Tunataka kuishi kwenye mazingira ya amani yaliyoepukana na vurugu."
Sheikh Abduwahab Mursal, katibu wa Baraza la Maimamu na Wahadhiri wa Kenya tawi la Wajir, alisema Ramadhani isiwe tu kwenye harakati baina ya imani tofauti ambako zimeanzia.
Pamoja na kufanya kazi pamoja na Wakristo kwenye kaunti hiyo kuimarisha mdahala wa amani, maulamaa wa Kiislamu lazima wabebe jukumu la ziada la kuhakikisha kwamba mapigano kati ya koo hayarejei tena, alisema.
"Tunajilinda dhidi ya wachochezi wa ghasia za kikoo na kidini," aliiambia Sabahi. "Katika kupambana na wenye siasa kali, maulamaa wa Kiislamu wanahubiri uvumilivu."
Vile vile, alisema kikosi cha ufuatiliaji kinachowajumuisha watu wenye dini tofauti kilichoundwa mwezi Septemba hukutana kila baada ya wiki mbili kuhakiki vitisho vilivyopo na vinavyojitokeza dhidi ya kuishi kwa amani katika ya Wakristo na Waislamu. Kikosi hicho kiliundwa baada ya mfululizo wa mashamulizi ya kigaidi dhidi ya raia katika kaunti hiyo, alisema.
Mheshimiwa Rueben Njue, mkuu wa Kanisa la Kianglikana la Kenya huko Wajir, alisema Wakristo wameridhishwa na msaada unaoendelea kutoka kwa Waislamu.
"Kumekuwa na mashambulizi yanayowalenga Wakristo, lakini katika baadhi ya matukio hayo, jamii ya Waislamu imeshirikiana na polisi na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa," alisema. "Ishara hizi zinathibitisha kwamba jamii kubwa si sehemu ya wahalifu wachache wanaoitumia vibaya dini."
Njue aliwashajiisha Wakristo kukubali mialiko ya kushiriki futari ya Ramadhani na majirani zao wa Kiislamu.
"Kugawana ni jambo zuri kwani kunaimarisha mafungamano yaliyopo," alisema. "Vile vile tunawatolea wito Wakristo kuwaheshimu Waislamu na ibada zao."
Rachel Nginya, msusi wa nywele mwenye umri wa miaka 33 mjini Wajir, aliiambia Sabahi kwamba majirani zake wa Kiislamu wanampa chakula takribani kila jioni.
"Majirani hao wanasisitiza nami siwezi kukikataa chakula chao. Ninashukuru sana kuwa nao," aliiambia Sabahi.

No comments:

Post a Comment

KARIBU