..

..
.

Wednesday, 28 November 2012

Maandamano yaendelea Misri

Maelfu ya waandamanaji katika uwanja wa Tahrir 
Polisi nchini Misri wametumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya maelfu ya waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo ikiwa ni katika kupinga hatua ya Rais Mohammed Mursi kujilimbikizia mamlaka zaidi.

Waandamanaji hao wanamtaka Rais Mursi abatilishe msimamo wake huo. Idadi kubwa ya wananchi wa Misri wameendelea kuandamana katika uwanja wa Tahrir, Cairo na mjini Alexandria pamoja na majimbo mengine 27 ya nchi hiyo, na hivyo kufanya hiyo kuwa idadi kubwa kabisa kukusanyika tangu kuzuka kwa mzozo huo. Maafisa wa usalama wamesema katika maeneo mengine ya nchi hiyo wananchi waliokasirishwa na hatua hiyo ya Rais Mursi walivamia makao makuu ya chama cha kiongozi huyo cha Udugu wa Kiislamu.
Mursi afananishwa na Farao
Wananchi hao wamemuita Rais Mursi dikteta na Farao mpya baada ya msimamo huo alioutangaza juma lililopita.
Rais wa Misri, Mohammed Mursi
                                            Rais wa Misri, Mohammed Mursi
Miongoni mwa hatua alizotangaza ni pamoja na kuipiga marufuku mahakama kutengua mamlaka aliyojiongezea au maamuzi mengine atakayoyachukua. Wengi wa wananchi waliompigia kura Rais Musri wameungana na wenzao kupinga hatua ya kiongozi huyo, katika maandamano yanayoonekana kufanana na yale yaliomuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Hosni Mubarak mwaka uliopita.
Hadi sasa watu watatu wameuawa kutokana na ghasia zilizozuka baina ya wapinzani wa Rais Mursi na wafuasi wake, tangu kiongozi huyo alipotangaza msimamo wake huo. Aidha, kwa upande mwingine maandamano mengine ya kumuunga mkono Rais Mursi yaliyokuwa yafanywe na chama cha Udugu wa Kiislamu mjini Cairo, yameahirishwa, ili kuzuia uwezekano wa kutokea machafuko. Hata hivyo, Rais Mursi ametetea msimamo wake akisema kuwa ni wa muda tu. Mzozo huo ni mkubwa kutokea tangu Rais Mursi achukue madaraka mwezi Juni mwaka huu.
Marekani inaufatilia mzozo wa Misri
Wakati huo huo, Marekani imesema inaufatilia kwa karibu mzozo wa Misri. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Victoria Nuland amesema hali nchini humo inazidi kuwa ya wasiwasi na kwamba bado hawajui matokeo ya maandamano hayo yatakavyokuwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland
                           Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland
Nuland amesisitiza kuwa Marekani inataka kuiona Misri inaendelea katika njia sahihi ya mageuzi ili kuhakikisha fedha zozote zinatolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF zinasaidia kwei utulivu na kuinua uchumi kwa kuzingatia kanuni za soko.
Inahofiwa huenda mzozo huo ukadhoofisha uchumi wa Misri ambao ulikuwa katika hatua za kuchipuka kufuatia mpango wa awali kufikiwa wiki iliyopita wa kupatiwa Dola bilioni 4.8 na IMF. Hata hivyo, IMF imesema Misri itaendelea kuzipata fedha hizo, licha ya mzozo huo iwapo hapatakuwa na mabadiliko makubwa katika ahadi zake za mageuzi.

No comments:

Post a Comment

KARIBU