MOJAWAPO ya sifa kubwa atakayokumbukwa nayo Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kutoa kauli tata ambazo hubakia katika mjadala kwa muda mrefu.
Tofauti
kidogo na kauli za hawali safari hii kauli yake imeondoka na vigogo wa
chama hicho na kuwatupa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za
uongozi wa jumuiya za chama na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Habari kutoka ndani ya NEC, ziliwataja walioenguliwa kuwa ni pamoja na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe.
Mbali ya hao, hasira za mwenyekiti huyo wa chama tawala zimemwangukia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Wengine waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Ludewa, Deo Filukunjombe. Wabunge hao ni miongoni mwa waliotia saini kutaka Waziri Mkuu Pinda ang’oke. Duru za siasa zinasema kuwa msimamo wa wabunge hao kuhusu Pinda, ndio ulisababisha wakatwe kuwania NEC.Athari za saini za kutaka kumng’oa Pinda ambazo zilisababisha Baraza la Mawaziri lipanguliwe na kuundwa upya, zimeonekana pia kumgusa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, ambaye ametupwa nje kuwania nafasi ya uenyekiti wa wazazi CCM taifa.
Hali ya mkosi bado inaendelea kumwandama Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Antony Diallo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza aliyekuwa akitetea nafasi yake, Clement Mabina ambao nao majina yao yamengolewa.
Wakati vigogo hao wakiugulia machungu ya kutoswa, Rais Kikwete ametoa kauli nzito ambayo moja kwa moja inaonekana kuwalenga wahanga hao ya kutaka wagombea waliopata kutoa kauli za vitisho dhidi ya chama hicho kufanya kile walichokusudia kukifanya.
Akizungumza kwa ukali, Kikwete ambaye juzi alitamba akisema CCM haitakufa kama inavyotabiriwa na baadhi ya watu, alihitimisha kauli yake kwa kusema watu wenye kauli za namna hiyo walikuwa hawafai kuendelea kuwa wanachama wa chama hicho.
Alisema
hivi sasa wagombea wengi wamekuwa wakijitokeza kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na kung’ang’ania kupata ushindi kiasi
cha wengine kufikia hatua ya kutoa kauli za vitisho kwa kusema
wasipopata nafasi ‘patachimbika’.
“Inashangaza kuona kugombea NEC tu watu wanataka kuuana, wanakimbilia nini huko ndani?” alihoji Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kama kuna wagombea ambao watajitoa ndani ya CCM na kuhamia chama kingine kutokana na majina yao kutopendekezwa, wajitoe.
Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa ukali, alisema anajua suala la kuwaengua baadhi ya wagombea litazua mjadala, lakini nia ya chama ni njema katika kuleta sura mpya na uhai.
“Kufanya
hivyo ni pamoja na kupata viongozi watakaokiletea chama ushindi katika
chaguzi za Serikali za Mitaa 2014 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,
hivyo lazima watu hao watambue kuwa kazi wanayoifanya ni kuunda timu ya
ushindi wa chama na si wa watu. “Najua kuna ndugu na marafiki
ambao hawatateuliwa kutokana na kujaa kwa nafasi na mapungufu na
madhaifu ambayo yalionekana baada ya Kamati ya Maadili kupitia majina
yao, hivyo wasione kama wameonewa bali wajue kama ndio utaratibu wa
chama wa kuhitaji viongozi shupavu, hodari na mwenye uwezo wa kukitetea
na kukipigania chama na kukipa ushindi,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment