..

..
.

Tuesday, 23 October 2012

MZEE MAKASA AISHI CHINI YA MTI MIAKA MITATU SASA



MWENYEWE AJIFANANISHA NA NABII AYUBU WA VITABU VITAKATIFU
ENEO la Buguruni Sokoni, katikati ya Barabara ya Uhuru iendayo na kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuna mti.
Mti huu upo jirani na Kituo cha Daladala Buguruni Sokoni kwa upande mmoja kuelekea makutano ya hiyo ya Uhuru na makutano ya Barabara ya Mandela kuelekea Ubungo, Tabata, Tandika au Uwanja wa Ndege.
Upande wa kulia wa mti huo kuna Kituo cha Polisi Buguruni.
Mti huo umekuwa ni hifadhi ya Mzee Omari Saidi Makasa kwa miaka mitatu sasa.

Chini ya mti, alipoketi Mzee Omari, utaona mifuko ya plastiki mikubwa iliyohifadhiwa vyema. Chini ya  mifuko hiyo kuna maboksi na vifurushi vidogo vidogo vitatu.
Kwa nyakati za usiku, mifuko hiyo ndiyo hugeuka kuwa shuka za Mzee Omari huku maboksi yakigeuka kitanda chake. Loh, maskini!
Makazi yake  yamezingirwa na shughuli mbalimbali za wafanyabiashara, waendesha magari, pikipiki na waenda kwa miguu.
Wakati wa foleni, mabasi makubwa au pikipiki huacha barabara na hupita karibu kabisa na miguu yake.
Jua kali siyo tatizo kwa mzee huyu, kwani kivuli cha mti humsitiri. Lakini, mvua humwamisha kwa muda na inapokoma … hakawii kurejea katika makazi yake.
Asubuhi, mchana, jioni, hata usiku wa manane, utamkuta akiwa ameketi au kulala chini ya mti huo, na amefanya hivyo kwa miaka mitatu sasa.
Mguu mmoja wa Mzee Omari una kidonda kikubwa kilichosababisha  mguu wake kuchimbika. Pia anasumbuliwa na ugonjwa wa mabusha ambao umewelemea.
Pamoja na hayo  yote, Mzee Omari anaonekana kuwa mwenye furaha ajabu,  akiyafananisha maisha yake na ya nabii Ayubu anayetajwa katika vitabu vya dini.
“Usiniulize kwa nini nakaa hapa, unamjua Mtume Ayubu? Si alipatwa na madonda mwili mzima, lakini akapona? Halafu akawa mzuri tena, basi na mimi ni hivyo hivyo,”alisema.
Mzee Omari ( 72),  anaanza kwa kusimulia kwa ufasaha hadithi ya Ayubu, akisema kuwa pamoja na watu kumcheka nabii huyo wakimtaka amkufuru Mungu, baadaye nabii huyo alipona na kuongezewa mali zake maradufu.
Anasema kuwa kama hilo lilitokea kwa nabii Ayubu, basi hata yeye anatumaini kuwa ipo siku ataishi maisha mazuri.
Akieleza kisa cha kuishi chini ya mti huo kwa muda wote huo anasema kuwa alianza maisha ya kutangatanga baada ya kupunguzwa kazi katika Kiwanda cha Useremala cha TACOMA.
Anadai kuwa kiwanda hicho ni cha zamani na kilifungwa mwaka 1989 wakati ambapo alipata matatizo katika mguu wake.
“Chanzo cha kupata kidonda hiki ni kujikwaruza na mbao.  Nashangaa sana ile mbao ilinikwaruza tu bila hata kunitoa damu, lakini kidonda kimekuwa hadi kufikia hivi,”anasimulia huku akitandika kipande cha boksi chini na kunilazimisha niketi naye.
 Anasema kuwa baada ya kupunguzwa kazi, alirudi kijijini kwao Dole, Wilaya ya Kondoa, lakini kidonda chake kilizidi uchimbika na aliamua kurejea Dar es Salaam kwa matibabu.
Mzee Omar anadai kuwa madaktari hawakumpa huduma bora na hiyo ndiyo sababu iliyosababisha kidonda chake kuwa sugu.
“Siku hizi hakuna madaktari, madaktari walikuwepo zamani. Madaktari wa sasa wanakupa dawa, badala ya kukuponya, inaongeza wadudu kwenye kidonda,” anasema.
Mzeehuyo anasema kwamba hataki kwenda hospitali yeyote, hata kama ni ya gharama nafuu, labda ikiwa nje ya nchi.
“Hata unipe milioni moja niende hospitali,  siwezi kwenda hospitali za Tanzania, naapa! Labda iwe Ulaya,” anasema.
 Anafafanua kuwa hata anapougua homa, kichwa au malaria katu hatumii dawa za hospitali, badala yake hujitibu kwa majani ya mti wa mwarobaini uliopo katika Kituo cha Buguruni Sokoni.
Tofauti na wazee wengi wasio na makazi jijini Dar es Salaam, Mzee Omar haombi fedha kwa kuweka kopo au bakuli mbele, wala hatamki neno lolote la kuomba msaada kwa wapita njia.
Hata hivyo, anapata milo yote miwili ya siku.
“Siombi mtu hela, wala sina haja ya kuomba. Mungu ananilisha hapa asubuhi na mchana. Ningetaka kula na usiku ningekula, lakini usiku huwa sisikii njaa,” anasema.
Anasema kuwa maisha yake ni kama ya Ayubu, hivyo Mungu amekuwa akimtendea miujiza na wasamaria wema wamekuwa wakimpa chochote walichonacho, bila hata ya kuwaomba.
“Watu wema wanaopita na magari wakiniona wananisaidia, utakuta wanampa hela muuza maji au mmachinga yeyote ananiletea,” anasema.
Anabainisha kuwa hajawahi kukosa mlo hata siku moja kwa muda wa miaka mitatu aliyoishi chini ya mti huo.
Mzee Omar anasemakuwa  Mungu alimjalia watoto wawili wa kiume ambao kwa bahati mbaya wote wamefariki na  baadaye alitengana na mke wake.
“Ndugu ninao, lakini wapo mbali sana huko vijijini Kondoa, hapa Dar nipo peke yangu,” anasema.
 Anabainisha kuwa anamiliki mashamba matatu makubwa kijijini kwake, lakini anashindwa kwenda kuyasimamia kwa sababu anasubiri muujiza wa kidonda chake kupona hapa hapa jijini.
Mpiga debe wa Kituo cha Buguruni Sokoni, Salum Baker anasema kuwa amemfahamu Mzee Omar kwa muda wa miaka saba tangu alipokuwa akiishi Buguruni kwa Mama Madenge.
“Namfahamu huyu mzee, zamani alikuwa anaishi kwa mama Madenge, baadaye akahamia kwenye mti ule pale karibu na kwa fundi cherehani, sasa hivi ndiyo yuko hapa ni mwaka wa tatu huu,” anasema Baker.
Anasema kuwa hana uhakika ni wapi mzee huyo anapopata fedha, lakini mara kwa mara amekuwa akimtuma kumnunulia bandeji za kufunga kidonda chake.
Mhudumu wa  Mesi ya Kituo cha Polisi Buguruni  Mercy Mjengwa, anasema kuwa anamfahamu mzee Omar kwa kuwa  ni mteja wake wa chai na chakula cha mchana kila siku.
“Hajawahi kuniomba nimpe chakula bure, kila siku ananunua. Asubuhi ananipa Sh500 kununua chai na maandazi au chapati, mchana ananipa Sh1500 za wali au ugali,” anasema Mercy.

No comments:

Post a Comment

KARIBU