TUMEZOEA kumsikia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa akitoa
kauli zenye utata na za kukanganya. Kauli zake mara nyingi huwa kali na
hulenga kujenga hofu kwa viongozi wa vyama vya upinzani. Kama
tulivyosema hapo juu, kauli zake zimezoeleka kiasi cha walengwa
kuzibeza, kuzipuuza na kuziita za kutishia nyau.
Ni kauli ambazo mara nyingi hutolewa kwa kukurupuka na pengine ndiyo maana huwa hazifuatiliwi, kwa maana ya kutekelezwa.
Ni
mara ngapi ametoa vitisho vya kufuta usajili wa baadhi ya vyama kwa
sababu ya kutoonyesha uhai na kushindwa kufanya kazi za kisiasa kama
mikutano ya hadhara, kufungua matawi, kushiriki katika chaguzi, kutafuta
wanachama, kufanya maandamano, makongamano na kadhalika? Ni mara ngapi
ametoa kauli zenye hisia kali dhidi ya vyama visivyokuwa na ofisi au
visivyoitisha mikutano ya wanachama au kuendesha chaguzi kwa njia za
kidemokrasia, kwa maana ya kuwaweka au kuwaondoa viongozi madarakani kwa
mujibu wa katiba za vyama hivyo?
Kama tulivyosema hapo juu,
kauli hizo hubezwa kwa sababu hazifuatiwi na utekelezaji. Ndiyo maana
miaka 20 tangu uanzishwe mfumo wa vyama vingi nchini, asilimia kubwa ya
vyama vilivyosajiliwa havina ofisi, havifanyi chaguzi za viongozi, kwa
maana ya vyama hivyo kuwekwa mifukoni na viongozi kama mali zao binafsi.
Vyama hivyo havifanyi kazi za kisiasa, haviko hai na havina wanachama
wa kuitwa wanachama. Ni vyama vilivyoanzishwa kwa mategemeo kwamba
Serikali ingetoa ruzuku kwa kila chama kilichosajiliwa kwa muda au
chenye usajili wa kudumu.
Inawezekana kwamba hutoa kauli kwa
hisia kali, tena kupitia vyombo vya habari ili kuonyesha na
kuuthibitishia umma na mamlaka iliyomteua kwamba anafanya kazi yake
vizuri na kwa ufanisi mkubwa. Lakini pia hufanya hivyo pengine kuonyesha
umuhimu wa kuwapo kwa ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Hicho
ni kitu gani kama siyo kuidhalilisha Ofisi ya Msajili?
Kwa
njia hiyo, amefanikiwa kuzima kelele za watu ambao wamekuwa wakitoa hoja
kwamba msajili huyo hafai kwa kuwa amejidhihirisha kwamba ni ‘simba wa
karatasi’ na kwamba ofisi hiyo ifutwe kwa sababu haina manufaa yoyote
kwa vyama vya siasa. Yapo madai mengine mengi kuhusu msajili huyo, ikiwa
ni pamoja na kusajili vyama mamluki ili kuvidhoofisha vyama makini na
kukisaidia chama tawala wakati wa chaguzi mbalimbali.
Hata
hivyo, pamoja na msajili huyo kuendeleza kauli zake za vitisho, vyama
makini vya kambi ya upinzani vimeshtushwa na kuichukulia kwa uzito
mkubwa kauli iliyotolewa juzi na Msajili Tendwa. Wakati wananchi bado
wanaomboleza kifo cha Mwandishi Daudi Mwangosi aliyeuawa kikatili na
polisi mwishoni mwa wiki mkoani Iringa, msajili huyo alitia chumvi
kwenye kidonda alipotishia kuvifuta vyama alivyodai vinakaidi amri ya
polisi ya kutofanya mikutano na maandamano, akidai kwamba mikutano hiyo
inakuwa na matukio ya vurugu na kusababisha vifo.
Tendwa
ambaye amekuwa akitishia kuvifuta vyama visivyofanya kazi za kisiasa
kama kufanya mikutano ya hadhara, juzi aligeuza kibao na kutishia
kukifuta Chadema, akidai kushangazwa na operesheni zake mikoani wakati
huu ambapo hakuna kampeni za uchaguzi. Tendwa yuleyule aliyetishia vyama
vilivyokuwa vinasubiri chaguzi ndipo vifanye kazi za kisiasa ndiye
yuleyule anayesema sasa hakuna kufanya kazi za kisiasa kama hakuna
shughuli za uchaguzi.
Huyo ndiye John Tendwa anayezuia
vyama vya upinzani kufanya shughuli za kisiasa kwa kisingizio cha kuwapo
Sensa, huku akikaa kimya siyo tu wakati chama tawala kikiendelea na
kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Bububu, bali pia kikiendelea na
mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake nchi nzima kwa wagombea wake
kuchukua na kurudisha fomu kwa nderemo na bashasha. Huyo ndiye Tendwa
aliyesema juzi baada ya mauaji ya Mwandishi Mwangosi kuwa, polisi
wanaporusha mabomu hawakusudii kuua watu, isipokuwa hivyo ndivyo
vitendea kazi vyao. Huyo ndiye John Tendwa.
No comments:
Post a Comment