..

..
.

Thursday, 20 September 2012

RAIS KIKWETE AKANA KUMUUZIA GEORGE BUSH ENEO LA KIGAMBONI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao amewaeleza kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye maendeleo.

Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki zao zote.

Daraja hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo unaweza kupungua na kubakia miezi 30.

Daraja hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 680 linagharimiwa kwa pamoja na Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60 na Serikali asilimia 40.

Daraja hilo ambalo litakuwa na jumla ya barabara za kupitisha magari sita kwa wakati mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China ambayo ni China Railway Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni ya Misri.

Daraja hilo litapunguza adha ya usafiri kati ya Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa sasa unategemea vivuko, ama boti ndogo, mitumbwi ama wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52. Kwa uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum kwenye daraja hilo pamoja na waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote ambao wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni watalipwa haki na stahiki zao.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.

No comments:

Post a Comment

KARIBU