..

..
.

Sunday 26 August 2012

YAFANYA MKUTANO MKUBWA IGUNGA KUSHUKURU WAPIGAKURA,DK SLAA AIONYA CCM IKIKATA RUFAA ITAUMBUKA



Katibu Mkuu wa Chamacha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa akiwahutubia wananchi wa mji wa Igunga na vitongoji vyake, katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi kwa ushiriki wao katika kufanikisha kesi ya uchaguzi wa jimbo hilo, uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Igunga jana.
Na abdullrahman Yusuph
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilitikisa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ikiwa ni mara ya kwanza tangu Mahakama Kuu Kanda Tabora kutengua ubunge wa Dk Dalaly Kafumu wa Chama Cha Mapinduzi, huku kikiionya CCM kuwa kitaumbuka iwapo kitakata rufaa kwa uamuzi huo wa mahakama.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Sokoine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema CCM kisithubutu kukata rufaa kwani kitaumbuka kwa kuwa kilicheza faulo nyingi katika uchaguzi huo.

Alisema ameshangazwa na kauli ya CCM kusema kuwa kitakata rufaa katika kesi hiyo wakati kisheria, kwa kesi za uchaguzi na pia katika hatua hiyo chama hakina nafasi yoyote bali mgombea au mwanachama wa chama husika, ndiye anayeweza kwenda mahakamani kufungua kesi na kupinga.

Katika mkutano huo uliofurika maelfu ya wanachama na washabiki wa wa chama hicho, Dk Slaa alisema kuwa  Chadema kitakiangusha vibaya CCM hata ikiwa uchaguzi katika Jimbo la Igunga utarudiwa.

Huku akitoa mifano mbalimbali ya jinsi baadhi ya wanachama wa CCM walivyokuwa wakitoa rushwa, Dk Slaa alimtuhumu Mweka Hazina wa chama hicho, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi kwamba alikuwa kinara wa kutoa rushwa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga Oktoba mwaka uliopita.

“Chadema imejipanga kwa rufaa hiyo ya CCM ikiwa ni pamoja na kufungua kesi nyingine dhidi ya vigogo wa CCM, walioshiriki katika kampeni za uchaguzi huo,”alisema Dk Slaa.

Dk Slaa pia alimponda Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akieleza kuwa mdomo wake umemponza kwa sababu alikuwa akizungumza mambo ambayo hakujua madhara yake.

Wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali wa Mahakama Kuu alisema moja ya hoja saba zilizotolewa na Chadema ambayo mahakama iliikubali ni ile ya Mukama kudai Chadema kilipeleka  makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga.

Dk Slaa alisema: “Mukama alikurupuka kwa kutamka maneno bila kufanya utafiti hali iliyosababisha CCM kupoteza jimbo.”

Alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa suala la CCM kuingiza silaha ndani ya nchi, bila kibali wala leseni na kuwapatia vijana wake mafunzo katika kambi za Ilemo, Iramba mkoani Singida linamhusu mwenyekiti wa chama hicho na siyo mtu mwingine.

Alidai kuwa wakati wa uchaguzi wa Igunga, vijana hao walikuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi akisisitiza kuwa suala hilo linamhusu mwenyekiti wa chama hicho akimtaka atoe majibu na ufafanuzi juu ya hilo.

Dk Slaa alisema kuwa siku ya jana ilikuwa ni kwa ajili ya wananchi wa Igunga kusherehekea na kupongezana kwa mshikamano waliouonyesha wakati wote wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, huku akitoa pongezi kwa mawakili waliosimamia kesi hiyo kwa kuiwakilisha vyema Chadema katika kesi hiyo.

Naye upande wake aliyekuwa mgombea wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Igunga Oktoba mwaka uliopita, Joseph Kashindye aliwashukuru wananchi walioiunga mkono Chadema akieleza kuwa wameonyesha ushirikiano mkubwa uliokipa ushindi chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kashindye aliwashukuru pia wananchi wa Igunga kwa kukichangia Chadema Sh6 milioni zilizosaidia kulipia gharama za kesi hiyo pamoja na malazi kwa mashahidi mbalimbali waliotoa ushahidi kwenye kesi dhidi ya CCM iliyotolewa hukumu wiki iliyopita kwa kutengua ushindi wa Dk Dalaly Kafumu wa CCM.

“Mahakama imetenda haki kwa kuwa imetoa hukumu ya haki…, nimeamini kuwa haki ya mtu haipotei. Awali nilidhani kuwa mahakama ni mali ya CCM kumbe si kweli,” alisema Kashindye na kushangiliwa na mamia ya watu waliofurika katika uwanja huo.

No comments:

Post a Comment

KARIBU