..

..
.

Tuesday, July 10, 2012

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MIGOMO SEHEMU ZA KAZI

Kamishna wa Kazi Msaidizi, Bwana Josephat Lugakingira akitoa Tamko la Serikali kuhusu migomo sehemu za kazi jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la kuitishwa migomo isiyozingatia taratibu zilizowekwa kisheria.

Kwa mujibu wa kifungu cha 80(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6/2004 ili mgomo uwe halali ni budi mambo yafutayo yazingatiwe:
  1. Ni lazima kuwepo na mgogoro wa maslahi baina ya wafanyakazi na mwajiri.
  1. Mgogoro huo uwe umeishawasilishwa kwa kutumia fomu maalum katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
  1. Mgogoro uwe haujapatiwa ufumbuzi baada ya siku thelathini (30) kupita tangu ulipopokelewa na Tume au katika muda wa siku thelathini za ziada zilizoongezwa na Tume.
  1. Mgogoro uwe haujapokelewa na Tume au katika muda wa siku thelathini zilizoongezwa na Tume.
  1. Mgomo uwe umeitishwa na Chama cha Wafanyakazi na kura imepigwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Wafanyakazi husika na wengi wa wanachama wawe wanaunga mkono.
  1. Taarifa ya masaa arobaini na nane (48) itolewe kwa mwajiri ikielezea nia ya wafanyakazi kugoma.
Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 76(1) cha sheria hiyo hiyo wafanyakazi walio katika huduma muhimu hawaruhusiwi kugoma isipokuwa tu baada ya kukidhi vigezo kadhaa vinavyosimamiwa na kamati ya huduma muhimu.

Kupitia gazeti la Mwananchi la tarehe 09/07/2012 Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Geita kimeazimia kufanya mgomo usio na kikomo kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni madai ya muda mrefu.

Tayari Chama cha Walimu Tanzania kimeishawasilisha mgogoro katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi – Dar es Salaam wenye namba za usajili CMA/DSM.ILA/369/12 na Tume inaendelea kuushughulikia.

Tunachukua fursa hii kuwataarifu wafanyakazi wote kuwa migomo ambayo si halali inamadhara yake ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika.

Mgomo uliozungumziwa kupitia gazeti la Mwananchi ni BATILI.  Hivyo Serikali inawataka wahusika wote kutojihusisha na vitendo vya uvunjaji wa sheria na badala yake Sheria na Kanuni zinazotawala mahusiano sehemu za kazi ziheshimiwe na kuzingatiwa.

No comments:

Post a Comment

KARIBU