Thursday, 5 July 2012
TAARIFA MPYA ZAELEZA YUKO UJERUMANI SI AFRIKA KUSINI, RAFIKI YAKE ATOA USHUHUDA MPYA WA JINSI ALIVYOTEKWA
WAKATI ikielezwa kwamba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka anatibiwa Afrika Kusini, kuna taarifa kwamba amelazwa katika hospitali moja ya huko Ujerumani.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa Dk Ulimboka alipelekwa Afrika Kusini lakini alikaa kwa muda mfupi tu kabla ya kupelekwa Ujerumani anakoendelea na matibabu yake sasa.
Awali, jopo la madaktari waliokuwa wanamtibu Dk Ulimboka hapa nchini lilieleza kuwa baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, waliamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
“Ni kweli alikwenda kwanza Afrika Kusini, lakini hapo alipita tu. Ndege ilitua na akaunganisha ndege nyingine kwenda Ujerumani,” kilisema chanzo kimoja cha habari.
Hata hivyo wakati chanzo hicho kikieleza hivyo, mmoja wa wanafamilia yake, alisema: “Sisi katika level (ngazi) ya familia tunajua yuko Afrika Kusini lakini hii haiwazuii madaktari kumhamishia kwenye hospitali nyingine wanayoona inafaa.”
Mwanafamilia huyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema suala la Dk Ulimboka kuhamishiwa Ujerumani si la ajabu kwani anachotafuta ni matibabu ya uhakika.
Alipoulizwa kuhusu habari hizo, Kiongozi wa Jopo la Madaktari waliokuwa wakimtibu, Profesa Joseph Kahamba alisema: Mimi ndiyo kwanza nasikia, lakini kwa nature (aina) ya tukio lake, si vyema ikaanikwa amepelekwa wapi. Pia si vizuri ikaelezwa yuko wapi ingawa tayari watu wanajua yuko Afrika Kusini.”
“Kama kiongozi wa jopo la madaktari wanaomtibu Dk Ulimboka ninajua kwamba yuko Afrika Kusini ingawa hata hiyo taarifa tusingependa watu waijue kwa jinsi tukio lilivyokuwa.”
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alipoulizwa juu ya suala hilo alipinga na kusema; “Habari za aina hiyo mtakuwa mnazipata nyingi, najua mtaandika, ndiyo maana mnaandika madaktari Muhimbili wanafanya kazi wakati si kweli”.
Alisisitiza kuwa Dk Ulimboka yupo Afrika Kusini anakopatiwa matibabu na kusisitiza kuwa habari alizokuwa nazo tangu juzi jioni ni kwamba anaendelea vizuri.
Katibu wa Chama cha Taifa cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick Kabangila alipoulizwa juu ya hali ya Dk Ulimboka alisema kwa mujibu wa taarifa za juzi jioni alikuwa anaendelea vizuri.
Alipoulizwa juu ya taarifa za kupelekwa Ujerumani aliguna kisha akasema: “Naomba ieleweke kuwa yupo Afrika ya Kusini kwa matibabu.
Rafiki asimulia mkasa
Rafiki wa karibu wa Dk Ulimboka aliyekuwa naye wakati mkasa wa kutekwa ukitokea, Dk. Deogratius Michael ameelezea tukio zima lilivyotokea na kusema ulikuwa wa kitaalamu na ulifanywa na watu wenye ujuzi na mambo hayo.
Dk Deogratius alisema jana kwamba siku ya tukio walikuwa wametokea kwenye msiba wa ndugu wa mwalimu wao Profesa Yongolo na baada ya msiba walikwenda Viwanja vya Leaders saa moja usiku kuangalia taarifa ya habari na mambo mengine.
Huko walikutana na madaktari wengine na ilipofika saa 4:00 usiku, Dk Ulimboka aliwaambia kwamba kuna jamaa alikuwa akimtafuta hivyo angependa kwenda kukutana naye.
“Tukamwuliza anamtafutia nini? Akatueleza kuwa kwa siku tatu huyo jamaa anamtafuta. Wenzangu wakasema asiende mwenyewe na mimi ndiyo nikamsindikiza. Mara ya kwanza huyo jamaa alisema anaitwa Abeid na alisema yuko Sterio, tukaenda huko hatukumkuta tukaenda Hugo hatukumkuta lakini baadaye tukakutana naye maeneo ya Barabara ya Tunis karibu na Ofisi za Ultimate Security.”
Dk Deogratius alisema wakati wakiendelea na mazungumzo, Abeid alikuwa akitaka kujua nini kinachotakiwa ili kutatua mgogoro uliopo wa madaktari.
“Wakati tunamalizia mazungumzo nilikwenda msalani, niliporudi Abeid alikuwa akizungumza na simu kila wakati, tuliendelea na mazungumzo hadi tukamaliza na kuanza kuagana,” alisema.
Alisema wakati wakiagana bado walikuwa wamekaa katika viti pamoja na Abeid... “Ghafla kuna watu walifika na kusema kuwa wanamtaka Dk Ulimboka. Walimchukua na kwenda naye katika gari. Walikuwa watano, walikuwa ‘giant’ (miili mikubwa) na ‘very skilled’ ( wenye uzoefu) wakamchukua Dk Ulimboka wakaenda naye kwenye gari,” alisema Dk Deogratius.
Alisema wakati huo Abeid alikuwa anakimbia hivyo akamkimbilia ili ampe namba yake ya simu ambayo ingemsaidia kwa mawasiliano.
“Alinipa namba yake nikampigia muda huohuo lakini nilipokuja kumpigia tena sikumpata na mpaka leo hapatikani,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo alimpigia mke wa Dk Ulimboka na kumweleza na pia alipiga simu polisi kuwaeleza.
“Nilikwenda polisi kutoa maelezo na nikawapa namba zangu za simu zote ili wanipigie kama watapata chochote, lakini mtu wa kwanza kunipigia asubuhi (kesho yake) alikuwa Juma Mgaza (aliyemwokota Dk Ulimboka) ambaye alinieleza kuwa kuna rafiki yangu amempa hiyo namba na kwamba yuko hoi amepigwa.”
Alisema baada ya kupata simu hiyo aliwasiliana na watetezi wa haki za binadamu ambao walimtaka waende pamoja na kwamba walipokuwa njiani kuelekea Kituo cha Polisi Bunju alipigiwa simu na polisi wa kituo hicho.
Kutokana na hali hiyo aliomba iundwe tume huru ikijumuisha wanasheria, madaktari na watu wengine ili ukweli ujulikane.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment