BIASHARA haramu ya usafirishaji binadamu hasa raia wa Somalia na
Ethiopia kwenda nchini Afrika Kusini kupitia Tanzania, inazidi kushika
kasi mkoani Kilimanjaro ikihusisha wafanyabiashara wakubwa na vigogo wa
Serikali.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi
upande wa Kenya katika maeneo ya Kitobo, Taveta, Ilasiti na Loitokitoki,
umebaini kuwa zaidi ya Wahabeshi na Wasomali 1,200 wapo mpakani upande
wa nchi hiyo wakisubiri kuvuka, kuingia Tanzania.
Hata hivyo,
jitihada za Serikali kudhibiti biashara hiyo zinaonekana kama mchezo wa
kuigiza kutokana na ukweli kwamba wahamiaji haramu hao wanapokamatwa,
hurudishwa hadi mpakani na kuachwa upande wa Kenya, ambapo mawakala wa
wahamiaji hao haramu wakiwamo Watanzania huwakusanya tena na kuandaa
upya safari zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert
Boaz amekiri kuwa biashara hiyo kuzidi kushamiri akieleza kuwa ni
kutokana na baadhi ya wananchi kukosa uzalendo. Uchunguzi huo
uliofanywa wiki iliyopita umewezesha kupatikana kwa taarifa zinazodai
kwamba kinara wa biashara hiyo yupo Mombasa, Kenya.
Imedaiwa kuwa
kinara huyo huwalipa mawakala kati ya Dola 2,000 na 4,000 za Marekani
ambazo ni sawa na kati ya Sh3 milioni na Sh6 milioni kwa kila mhamiaji
haramu anayesafirishwa kutoka Mombasa hadi Malawi.
Habari
zinaeleza kuwa wahamiaji hao haramu huingia mkoani Kilimanjaro kupitia
njia za panya za mipakani zilizopo katika Wilaya za Siha, Rombo, Same,
Mwanga, Moshi Vijijini na kuhifadhiwa kwenye nyumba za wenyeji. “Sasa
kuhifadhi wahamiaji haramu ni 'deal' (biashara), kwa sababu wenyeji
wanalipwa kati ya Sh100,000 hadi Sh500,000 kwa siku kulingana na idadi
ya wahamiaji,” alidokeza mkazi mmoja wa Tarakea, Rombo.
Maeneo
ambayo yamekithiri kwa kuingiza wahamiaji hao ni Tarakea wilayani Rombo,
Kitobo, Kilototoni, Mabungo Moshi Vijijini, Chekereni na Kifaru
wilayani Mwanga.
Mbali na jitihada za vyombo vya dola kudhibiti
biashara hiyo, wahamiaji hao bado wamekuwa wakiingia mkoani Kilimanjaro,
huku wengine wakifichwa katika mapori wilayani Mwanga.
Wahamiaji
wanavyoingia Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa kwa maeneo
ya Moshi Vijijini, wahamiaji hao haramu huanzia eneo la Kitobo na
kusafirishwa kwa pikipiki ambazo hulipiwa Sh20,000 kwa kila safari.
Wahamiaji
wengine haramu hupelekwa, kuhifadhiwa katika nyumba zilizopo Mabungo,
Kifaru na Kilototoni, ambapo huhudumiwa kwa kupewa mikate mikavu, maji
ya kunywa ya chupa na chakula kingine.
Wilayani Rombo, wahamiaji
haramu hao huingizwa nchini kupitia Vijiji vya Nayeme, Leto na Kikelelwa
na kuhifadhiwa kwa muda katika nyumba za wenyeji kabla ya kusafirishwa
hadi Chekereni.
“Kutoka hapa Rombo wanasafirishwa kwa magari aina
ya Toyota Noah, mengine yanamilikiwa na polisi na pia malori aina ya
Fuso… Hii ni deal (biashara) ya watu wazito,” alidokeza mkazi mmoja
aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu za kiusalama.
Mbali na
wilaya hizo, katika Wilaya ya Mwanga, wahamiaji haramu huhifadhiwa
katika Vijiji vya Kivisini, Ziwa Jipe,Toloha na husafirishwa hadi karibu
na Hifadhi ya Mkomazi au Ndungu.
Njia mpya
Uchunguzi
umebaini pia njia mpya inayotumika kuwaingiza wahamiaji hao, ambayo
vyombo vya ulinzi na usalama havijaweza kuibaini ikianzia Mwanga kwenda
Nyumba ya Mungu, hadi Orkasment wilayani Simanjiro.
No comments:
Post a Comment