Viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam wametakiwa kutumia vema nyadhifa
na fursa walizonazo katika kuhakikisha kuwa waamini wao wanatii sheria
bila ya kushurutishwa.
Wito huo umetolewa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ally Hassan
Mwinyi wakati alipokuwa akizindua kampeni ya utii wa Sheria Bila Shuruti
kwa viongozi wa dini za Kiislam na Kikristo.
Mhe. Mwinyi amewataka viongozi hao kutumia fursa wanazozipata kupitia
Ibada na Swala katika kuwahubiria waamini wao kuhusiana na suala zima la
kutii Sheria bila ya kushurutishwa.
Amesema kuwa kwa kuwa viongozi hao wa dini ndio watu pekee ambao
wanakuwa na watu wote katika nyakati zote za maisha yao bila kujali
itikadi wala kabila, hivyo ni rahisi kwao kuwashawishi waumini hao watii
sheria bila ya kushurutishwa kutokana na imani waliyonayo juu yao.
Aliongeza kuwa endapo kila kiongozi atafanikiwa kuwashawishi waamini
wake watii sheria bila ya kushurutishwa, nao wakatii , basi ni wazi kuwa
uhalifu utapungua nchini na amani yetu itadumu daima.
Alhaji Mwinyi pia amewasifu viongozi hao wa dini kwa hatua waliyoichukua
ya kuweza kukaa pamoja bila ya kujali itikadi zao na kufikia muafaka wa
kuanzisha kampeni hiyo ambayo ina lengo la kudumisha amani nchini.
Mhe. Mwinyi alitoa rai kwa taasisi za Kiserikali, Sekta binafsi pamoja
na mtu mmoja mmoja kuzingatia utii wa sheria bila ya kushurutishwa kwa
kufanya hivyo kutaleta tija kwa taifa.
“Watumishi wa Umma wakitii sheria bila ya kushurutishwa wananchi
watapata huduma kutoka kwa watumishi hao vizuri na kwa hivyo itaondoa
fikra potofu za kwamba watumishi wa Umma hawatekelezi wajibu wao mpaka
kwa kusukumwa”
Aidha Alhaji Mwinyi amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri
anayoifanya katika kukabiliana na uhalifu nchini ikiwa ni pamoja na
busara aliyoitumia katika kuwashawishi viongozi hao wa dini hata
wakafikia kukaa pamoja na kuanzisha kampeni hiyo.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wenzake, Sheik Issa Othman Issa amewataka
watanzania kupokea mafundisho mema yanayotolewa na viongozi wao wa dini
ili kujenga taifa bora na lenye kutii mamlaka zilizopo.
Sambamba na uzinduzi huo pia kulizinduliwa vitabu vya ‘Utii wa Sheria ni
Wajibu, kufuata sheria bila shuruti ni thawabu’ kilichoandaliwa na
Taasisi ya Kiislamu ya Mwinyi Baraka na kitabu cha ‘Baraka za utii bila
shuruti’ kilichotolewa na Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania.
Uzinduzi wa kampeni hiyo iliyokuwa na kauli mbiu ya’ Utii wa Sheria ni
Thawabu’ kwa upande wa Kiislamu na ‘Baraka za Utii wa Sheria’ kwa
upande wa Kikristo ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee na
kuhudhuriwa na viongozi wa dini zote mbili kutoka mikoa mbalimbali
nchini.
No comments:
Post a Comment