Tume
imepata nakala elfu mia tano za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977,
nakala elfu kumi za Katiba ya Zanzibar ya 1984 na nakala elfu mia tano
za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa kutambua kwamba
nyaraka hizi hazitoshi, na hata kama zikipatikana kwa wingi ni vigumu
kwa wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi, Tume imeandaa nyaraka
ambazo ni rahisi kuzisoma na kuzielewa.
Nyaraka
hizo ni Katiba ya Jamhuri ya 1977, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura
ya 83, kwa lugha nyepesi, Hadidu za Rejea, Program ya Elimu kwa Umma na
Utekelezaji wa Kazi za Tume. Nyaraka hizi tumeanza kuzisambaza na leo,
tunawakabidhi nyinyi nyaraka zote ili msaidie kuzitangaza na kuelemisha
wananchi. Aidha, Tume imeandaa vipeperushi kuhusu kazi za Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara.
Ndugu Wanahabari,
Hivi
karibuni Tume itaanza safari za mikoani. Tume imejigawa katika makundi
saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho
wa mwaka. Kila kundi litafanya kazi katika mkoa kwa wastani wa mwezi
mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume itatumia
muda mfupi. Tutaanza na mikoa minane ambayo ni Dodoma, Kagera, Kusini
Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Tunaomba
wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru, uwazi, bila
ya hofu yoyote na kwa utulivu. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu na
watoe maoni bila jazba au kubeza. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu sana
kusikiliza mawazo ya wengine hata kama hawakubaliani na mawazo hayo.
Lengo
letu kama Tume, ni kuhakikisha kuwa Watanzania kwa jumla wanatoa maoni
yao. Tungependa sana kama ingeliwezekana, kila Mtanzania apate fursa ya
kutoa maoni yake. Lakini, ukizingatia ukubwa wa nchi yetu na mazingira
halisi, ni wazi haitawezekana kuonana na kila mtu. Pamoja na hivyo, ni
kusudio letu kufanya kila linalowezekana kupata mawazo ambayo
yataonyesha matakwa, mategemeo na mahitaji ya Watanzania wote. Katika
upeo huo, basi tutafanya kila jitihada kwa njia mbali mbali kujaribu
kuhakikisha kwamba maoni ya Watanzania kwa ujumla yanawasilishwa na
kufanyiwa kazi vilivyo.
Pamoja
na mikutano mbali mbali itakayofanyika katika mikoa yote, tutakuwa na
mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa kutoka pande zote za ndani ya
nchi na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii kama
facebook, twitter na blogu na tovuti na pia kwa njia ya posta. Tunaomba
wananchi wajitahidi kutoa hoja badala ya malalamiko peke yake.
Mapendekezo ya mambo ya kuingia kwenye Katiba yatasaidia sana badala ya
malalamiko tu.
Tume,
kwa kiwango fulani imeanza kuratibu maoni ya wananchi yanayotolewa kwa
njia mbali mbali. Mwelekeo wa kubaini maeneo ya kufanyia kazi unaanza
kuonekana, hasa kuhusu taasisi za dola kama vile Serikali na vyombo
vyake vyote na madaraka ya viongozi na taasisi mbali mbali. Tume
inaomba maeneo mengine muhimu nayo yapewe uzito, hasa maeneo yaliyo
katika Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977. Sehemu hiyo ndiyo moyo wa Katiba. Yapo maeneo manne muhimu
ambayo Tume ingependa kupata maoni ya wananchi.
Eneo
la Kwanza, linahusu misingi ya Taifa. Misingi ndiyo nguzo ya utamaduni
wa nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya nidhamu ya nchi na
wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya maadili ya nchi na wananchi wake.
Katiba yetu imetaja misingi mikuu kuwa ni uhuru, haki, udugu, amani,
demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote ingawa wananchi wana
uhuru wa kuabudu. Misingi hii ndiyo nguzo ya mshikamano na utulivu wa
wananchi. Baadhi ya watu wanasema ama misingi hii haitoshi au
imetelekezwa. Wengine wanasema inatosha. Tume ingependa kupata maoni
ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo
la Pili, ni kuhusu mamlaka ya wananchi. Katiba ya sasa inaeleza kwamba
wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na msukumo mkubwa wa mchakato huu
wa kupata Katiba Mpya ni matakwa ya kuwawezesha wananchi kutunga Katiba
yao. Lakini kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa,
wanasema mamlaka ya taasisi za dola kama vile Serikali, Bunge, Mahakama,
Tume mbali mbali za kikatiba, na hata Vyama vya Siasa, yamefafanuliwa.
Lakini mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa na wala hakuna utaratibu wa
kuyatumia madaraka hayo. Wanasema wananchi wanatumiwa tu kisiasa wakati
mamlaka yao yote yameporwa. Wengine wanasema mamlaka hayo yapo
isipokuwa wananchi wameyakasimu kwa taasisi mbali mbali. Tume ingependa
kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo
la Tatu, ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za
Serikali. Malengo hayo yameelezwa vizuri sana katika Ibara ya 9 ya
Katiba. Baadhi yake ni:-
· Kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
·
Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo
zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na
unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu
kumnyonya mtu mwingine;
· Kwamba mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi;
· Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.
·
Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo
ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha
umaskini, ujinga na maradhi;
·
Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza
kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya
watu wachache binafsi.
Malengo
haya ndiyo ndoto (vision) ya wananchi. Malengo haya ndiyo yanajumuisha
matumaini ya Watanzania kuhusu aina ya Tanzania wanayoitaka. Mgawanyo
wa madaraka kwa mamlaka mbali mbali za dola unakusudiwa kuhakikisha
kwamba malengo haya yanafikiwa.
Baadhi
ya watu wanasema kuwa malengo haya yanatosha ila hayatekelezwi kwa
ukamilifu. Wengine wanasema kuwa hayatoshi katika zama hizi. Tume
ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu malengo muhimu ya Taifa. Tume
itapenda kufahamu ndoto za wananchi kuhusu rasilimali za Taifa na jinsi
ya kuzilinda, kuziendeleza na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi.
Tume
ingependa kusikia ndoto za wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi,
wafanya biashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee, vijana,
walemavu na kadhalika.
Eneo
la Nne, ni haki za binadamu na wajibu kwa jamii. Sehemu ya Tatu ya
Sura ya Kwanza ya Katiba ina orodha ndefu ya haki na wajibu muhimu kwa
raia. Baadhi ya watu wanasema haki hizi hazitoshi. Wengine wanasema
haki za mtu binafsi zinadhulumu haki za jamii na wengine wanasema haki
za binadamu zinaminywa au hazitekelezwi kwa ukamilifu au zinavunjwa.
Tume inapenda kupata maoni ya wananchi.
Ndugu Wanahabari,
Awamu
ya Pili ya uratibu na ukusanyaji wa maoni ya wananchi itafanyika
kupitia Mabaraza ya Katiba. Wakati huo, Tume itawaomba wananchi watoe
maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Kupitia kwenu, naomba wananchi
kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni katika awamu
zote mbili. Nawaomba wananchi kutoa mawazo yao kwa uwazi na bila ya
hofu yoyote. Tume itafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na
tunawahakikishia kwamba maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi,
asasi za kiraia na makundi mengine yote yataheshimiwa na kufanyiwa kazi
ipasavyo.
Ndugu Wanahabari,
Nimalizie
kwa kurudia tena kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kubwa katika
kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya. Pamoja na mambo mengine,
wananchi wa sehemu moja ya nchi watafahamu maoni ya wenzao katika sehemu
nyingine ya nchi. Naomba mlikubali jukumu hili ili kusaidia nchi ipate
Katiba Mpya iliyo nzuri.
No comments:
Post a Comment