Wakati
Bunge liko kwenye mchakato wa Bajeti ya 2012/13, yameanza kujitokeza
maneno na taarifa mbalimbali juu ya kupanda kwa mishahara ya watumishi
wa Umma wakiwemo Wabunge. Mathalani, siku ya Jumatano tarehe 20 Juni
2012, gazeti moja linatokalo kila siku lilikuwa na habari yenye kichwa
kisemacho “Mishahara ya Wabunge juu”.
Ofisi
ya Bunge imeona ni vyema kutoa ufafanuzi juu ya suala zima la
mishahara ya Wabunge ili umma uweze kuelimika ipasavyo juu ya taratibu
zinazotawala jambo hili kama ifuatavyo:
· Bajeti
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inajumuisha Fungu Na. 42 lenye Bajeti
ya Bunge bado haijasomwa Bungeni, na hivyo haiwezekani leo hii kueleza
kuwa kuna nyongeza ya bajeti inayohusu mishahara kwa Wabunge.
· Si
kweli kwamba mishahara ya Wabunge imeongezwa toka kiwango wanacholipwa
sasa, kwa kuwa mishahara yao kama ilivyo ya watumishi wote wa umma,
hurekebishwa kwa waraka maalum toka Ofisi ya Rais, na si Kamisheni au
Kamati yoyote ya Bunge.
· Waraka
wa mwisho wa toka Ofisi ya Rais unaotoa Masharti ya Kazi ya Mbunge
ulitolewa tarehe 25 Oktoba 2010, na kueleza kuwa Mbunge atalipwa
mshahara katika ngazi ya LSS (P) 2, na ni waraka huo unaotumika mpaka
sasa.
· Mapendekezo
ya ongezeko la 32% ya Bajeti ya Ofisi ya Bunge yaliyooneshwa kwenye
kitabu cha Bajeti namba 2, cha matumizi ya kawaida yaliyowasilishwa
mezani ni ya matumizi mengine ambayo hayana uhusiano na ongezeko la
mishahara.
Mwisho,
Ofisi ya Bunge wakati wote inathamini sana mchango wa vyombo vya
habari katika juhudi za kuelimisha umma juu ya kazi za chombo chao cha
uwakilishi. Hata hivyo, Ofisi inasikitishwa sana na habari za
upotoshaji zinazotolewa kwa lengo la kujenga chuki kati ya Wabunge na
watu wanao wawakilisha.
Kwa
mantiki hiyo, tunazidi kuwasihi Waandishi waandike habari au makala
baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu jambo husika na pale inapobidi
waweze kupata ufafanuzi toka Idara husika katika Ofisi ya Bunge, ili
kuepuka kuupotosha umma.
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941, DODOMA
No comments:
Post a Comment