"Hisia zangu sasa ni kwamba kila mtu serikalini na kwengineko duniani amefadhaishwa sana na kuendelea kwa ghasia nchini Syria," Kerry aliwaambia waandishi wa habari, akiwa na mwenzake wa Canada, John Baird. "Kuna mauaji ya kupindukia. Kuna ghasia za kupindukia. Na ni wazi kuwa tunataka kupata njia ya kusonga mbele."
"Kwa sasa tunatathmini," alisema. "Tunaangalia hatua gani, hasa hasa za kidiplomasia, zinaweza kuchukuliwa katika jitihada za kujaribu kupunguza ghasia hizo na kuishughulikia hali hii."
Mgawanyiko wa wazi
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta.
Waziri wa Ulinzi anayemaliza muda wake, Leon Panetta, na
Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi, Jenerali Martin Dempsey, waliliambia
bunge hapo Alhamis (07.02.2013) kwamba wao walishapendekeza kutoa msaada
wa kijeshi kwa waasi lakini wakapingwa na Rais Obama.Katika kuonesha kiwango gani serikali ya Obama imegawanyika juu ya namna ambavyo Marekani inapaswa kuzishughulikia ghasia hizo za Syria ambazo zimeshaua kiasi cha watu 60,000 kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, Panetta na Dempsey walisema kwamba wanaunga mkono kuwapa silaha waasi, lakini Rais Obama akatoa uamuzi wa mwisho wa kupinga hatua hiyo.
Serikali ya Marekani imepigania kipindi chote hiki kuja na sera ambayo itasaidia kumaliza umwagikaji damu na kuharakisha kuondoka madarakani kwa Rais Assad. Rais Obama alimtolea wito Assad kuondoka madarakani mwezi Agosti 2011, lakini Marekani imekataa kuunga mkono dhana yoyote ya kuingilia kijeshi, iwe kwa kufanya doria kwenye anga ya Syria kuzuia mashambulizi ya serikali au kwa kuwapa silaha za kisasa waasi.
Hofu ya utawala wa Obama
Rais Barack Obama (kulia).
Maafisa wa Marekani wamesema kwamba, tafauti na ilivyokuwa kwa
Libya, hakuna idhini ya Umoja wa Mataifa kwa Marekani kujiingiza moja
kwa moja kijeshi kama vile kuweka marufuku ya kuruka ndege. Maafisa hao
wanaamini kwamba mpango wowote wa kuwapa silaha waasi utaufanya mgogoro
huo kuwa wa kijeshi zaidi, ilhali unastahiki kutatuliwa kisiasa.Juu ya yote, kuna shaka kwamba ikiwa silaha hizo zitakuja kuangukia kwenye mikono ya magaidi au makundi ya wenye siasa kali, basi baadaye zitakuja kugeuzwa dhidi ya Israel au washirika wengine wa Marekani na maslahi ya nchi hiyo kwenye eneo hilo.
Kerry alisema hajui undani wote wa maamuzi ya ndani ya utawala wa Obama, lakini anaamini kunatakiwa kuwepo kwa suluhisho la haraka.
"Sijui mijadala iliyokuwapo Ikulu na nani alisema nini, na sitarudi nyuma. Huu ni utawala mpya sasa, kipindi cha pili cha rais, nami ni waziri mpya wa mambo ya nje na tutasonga mbele kutoka hapa tulipo." Alisema Kerry mwisho wa wiki yake ya kwanza katika kazi yake mpya.
Jeshi lapigania kuidhibiti Damascus
Rais Bashar al-Assad (kushoto) na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Nchini Syria kwenyewe, jeshi limeendelea kupambana kujaribu
kurudisha sehemu za barabara inayouzunguka mji wa Damascus kutoka kwa
waasi wanaokaribia kuuteka mji huo mkuu.Ndege za kivita ziliyashambulia maeneo kadhaa yanayouzunguka mji huo, na mapigano makali yalitokea katika makutano ya Hermalleh yaliyoko katika barabara hiyo, ambayo imetekwa na waasi.
Waasi walivunja ngome za serikali siku ya Jumatano, na kuteka sehemu za barabara hiyo, na maeneo yaliyoko umbali wa kilomita mbili kutoka vituo vya usalama katikati mwa mji wa Damascus.
Rais Assad amepoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya Syria, lakini vikosi vyake vikisaidiwa na mashambulizi ya angani, vimefanikiwa kuwazuia waasi kufika katikati mwa Damascus.
No comments:
Post a Comment