Katika Shehiya ya Magomeni, mkutano ulivunjika baada ya makundi mawili hasimu kuvurugana. Kundi moja linalosadikiwa kuungwa mkono na CCM linataka mfumo wa Muungano uliopo uendelee, yaani Muungano wenye Serikali mbili, wakati kundi la pili linalosadikiwa kuungwa mkono na CUF linataka Muungano wa mkataba na serikali tatu.
MIKUTANO
ya kukusanya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya imeingia dosari kisiwani
Unguja baada ya baadhi ya wanasiasa na wafuasi wao kuvamia mikutano hiyo na
kusababisha ghasia, huku baadhi ya watu wakijeruhiwa kwa kuchomwa visu.
Vurugu
hizo zilitokea mwanzoni mwa wiki katika shehiya za Mpendazoe na Magomeni katika
Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha kuahirishwa kwa mikutano hiyo kwa
kuhofia usalama wa wananchi. Tukio la baadhi ya watu kuchomwa visu katika
Shehiya ya Mpendazoe lilitokana na baadhi ya vijana kuvamia mkutano huo na
kufanya fujo.
Katika Shehiya ya Magomeni, mkutano ulivunjika baada ya makundi mawili hasimu kuvurugana. Kundi moja linalosadikiwa kuungwa mkono na CCM linataka mfumo wa Muungano uliopo uendelee, yaani Muungano wenye Serikali mbili, wakati kundi la pili linalosadikiwa kuungwa mkono na CUF linataka Muungano wa mkataba na serikali tatu.
Kutokana na Tume pengine kushindwa kutoa elimu ya kutosha kuhusu mchakato huo,
wananchi wengi visiwani humo wamekuwa na dhana potofu kuwa, kundi
litakaloonekana kutoa maoni mengi mbele ya Tume kuliko lingine ndilo litakuwa
limeshinda, hivyo Katiba itakayotungwa itazingatia zaidi maoni yaliyotolewa na
kundi hilo.
Vurugu zinazotokea katika mikutano mingi ya tume hiyo kwa kiasi kikubwa
zinachangiwa na hali hiyo ambayo imesababisha wanasiasa kuwasafirisha wafuasi
wao kutoka mbali na kuwaleta katika sehemu nyingine ambako mikutano hiyo
inafanyikia. Vurugu hizo pia zinasababishwa na wale wanaosafirishwa kutoka
sehemu za mbali kulazimisha kukaa mbele ya wenyeji waliowatangulia ili waweze
kutoa maoni kwa sababu Tume haina muda wa kutosha kusikiliza maoni ya wananchi
wote wanaotaka kutoa maoni yao.
Itakumbukwa kwamba Tume iliweza kugundua mbinu zinazofanywa na baadhi ya
viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii nchini, hasa Unguja na Pemba ambapo
wanawapa kwa maandishi wanachama na wafuasi wao maoni ya kusoma mbele ya Tume.
Tunaambiwa mbinu hizo hivi sasa
zimepamba moto, hasa baada ya kujikita kwa dhana kwamba wingi wa maoni
yatakayotolewa kwa Tume kuhusu jambo fulani ndiyo yatakayopewa uzito na Tume
hiyo katika kuandika rasimu ya Katiba Mpya.
Ni bahati mbaya kwamba Tume haijafanya juhudi za kutosha kuwaelimisha wananchi
ili watambue kwamba jukumu lake siyo tu kukusanya maoni ya wananchi, bali pia
kuyaratibu, kuyatathmini na kuyaainisha katika muktadha wa Katiba inayofaa
kulingana na matakwa ya wengi. Hapa lazima ieleweke kwamba maoni ya wengi
kuhusu jambo fulani siyo lazima yapokelewe na Tume kama itaonekana kwamba
yanakwenda kinyume na masilahi ya taifa.
Kwa mfano, pamoja na kwamba asilimia
80 ya wananchi waliotoa maoni yao walitaka mfumo wa chama kimoja uendelee, Tume
ya Nyalali ilipendekeza serikalini kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi siyo tu
kwa ajili ya kwenda na wakati, bali pia kwamba ndiyo ungesaidia kuhakikisha
unakuwapo mshikamano na umoja wa kitaifa.
Inasemekana kwamba baada ya matukio hayo ya shehiya za Magomeni na Mpendazoe,
Tume imelazimika kuuangukia uongozi wa Mkoa ili uingilie kati kwa kuhakikisha
unakuwapo ulinzi wa kutosha katika mikutano hiyo. Hatua hiyo imetokana na
vitendo vya baadhi ya wananchi, wakiwamo baadhi ya wanasiasa, wawakilishi na
wabunge kuwashambulia wajumbe wa tume hiyo kwa maneno ya vitisho na vya
kuwadhalilisha.
No comments:
Post a Comment