Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini
Watanzania bara wanaoishi Zanzibar wataanza kusajiliwa na kupewa vitambulisho maalum sawa na raia wa nje ya Tanzania wanaoishi Zanzibar.
Kwa Mujibu wa muswada wa marekebisho ya sheria ya Usajili ya Mzanzibari mkaazi namba 7 ya mwaka 2005 kazi ya kuwasajili itaanza kufanyika miezi mitatu baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo.
Muswada huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Ikulu) Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Oktoba 10 mwaka huu.
Kifungu cha 6A (1) cha muswada kimeleza kwamba kila mkazi asiyekuwa Mzanzibari atatakiwa kujisajili katika Ofisi ya usajili wa vitambilisho vya Mzanzibari mkazi.
Muswada huo umeleza kwamba zoezi hilo pia litawagusa raia wa kigeni ambao wanaishi Zanzibar na kufanya kazi au biashara.
Kifungu cha 6A (3) kimeleza aina ya wageni wanaotakiwa kusajili kwa mujibu wa sheria hiyo wanaofanyakzi Zanzibar ama kwenye taasisi ya umma au binafsi pamoja na wanaofanyabiashara visiwani humo.
“Muajiri wa mkazi asiyekuwa Mzanzibari atatakiwa kutoa taarifa za mtu huyo kwa mkurugenzi au afisa msajili ndani ya siku 60 kuanzia ajira yake au ikiwa ameajiriwa kabla ya kuanza kutumika kwa sheria hii,” umesisitiza muswada huo.
Aidha, muswada huo umefuta kifungu cha 7 na watu wote watakaosajiliwa watatakiwa kuchukuliwa alama za vidole badala ya kidole gumba kimoja kwa mujibu wa sheria hiyo.
Akizungumza na NIPASHE Mkurugenzi wa usajili wa Vitambulisho vya Uzanzibari mkazi Mohamed Juma Ame, alisema serikali imeamua kuwasajili watu hao baada ya kubainika kuwepo watu wanaopewa vitambulisho hivyo kinyemela.
Alisema kwamba hali hiyo imekuwa ikifanyika baada ya vitambulisho hivyo kuonekana kuwa ni nyenzo muhimu katika maisha ya kila siku hasa katika upatikanaji wa huduma za jamii.
Mohamed alisema sheria hiyo pia itasadia kuwatambua watu wanaoingia na kutoka Zanzibar maeneo wanayoushi na kazi wanazofanya Zanzibar.
Hivi karibuni Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakilalamika kuwa vijana wengi Zanzibar wameshindwa kunufaika na ajira katika sekta ya Utalii kutokana na kazi hizo kuvamiwa na wageni kutoka nje ya Zanzibar ikiwemo Tanzania bara
No comments:
Post a Comment