..

..
.

Tuesday 14 August 2012

YABAINIKA HAYUPO NYUMBANI, TAARIFA ZAKE ZAFANYWA SIRI, BABA, NDUGU, MARAFIKI WAGOMA KUZUNGUMZA



Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam juzi akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.Picha na Fidelis Felix
WINGU limegubika sakata la kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka siku moja baada ya kurejea nchini, huku watu wake wa karibu akiwamo baba mzazi, wakigoma kusema chochote kumhusu. Dk Ulimboka alirejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu kwa takriban mwezi mmoja na nusu, baada ya kutekwa, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo na Jiji la Dar es Salaam usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.
Ingawa wakati wa ugonjwa wake baadhi ya watu wake wa karibu walikuwa wakitoa maelezo mbalimbali, jana wote waligoma kusema chochote, huku jitihada za gazeti hili kumpata nyumbani kwake zikigonga mwamba.
Baba mzazi wa Dk Ulimboka, Stephen Mwaitenda aliweka wazi kuwa ni vigumu kumwona daktari huyo jana.
Takriban watu wote waliofika nyumbani kwa Mzee Mwaitenda jana kumjulia hali Dk Ulimboka waliambiwa kuwa hayupo nyumbani.
Mwaitenda alilieleza gazeti hili kuwa ana furaha kuwa mtoto wake alirejea nchini salama licha ya kupelekwa Afrika Kusini akiwa taabani kutokana na kipigo.
Alipotakiwa kueleza juu ya kile kilichompata, mtoto wake huyo alisema: "Mungu na Steven mwenyewe (Dk Ulimboka) ndio wanaojua kilichotokea."
Aliongeza: “Kweli nimefurahi kwamba mwanangu amerudi, lakini siwezi kuelezea nini kilimtokea alipotekwa," alisema Mwaitenda.
Alisema Dk Ulimboka hayupo nyumbani na hajui kwamba angerudi wakati gani. "Hata kama angekuwapo, ni vigumu kumwona," alisema.
Kauli ya Katibu wa Madaktari
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema madaktari walikuwa hawajaamua nini kingefuata baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini.
Alisema hata hivyo, daktari huyo anahitaji muda wa kupumzika kwanza na familia yake.
“Aliporudi jana (juzi) alitumia muda wake kukaa na familia yake, mpaka sasa hatujajua hatua inayofuata. Dk Ulimboka atazungumza wakati mwafaka ukifika,” alisema Dk Chitage.
Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi hakutaka kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa alikuwa mkutanoni.
Dk Mkopi alitoa kauli hiyo baada ya daktari aliyemtibu Dk Ulimboka wakati wa tukio la kutekwa, Profesa Joseph Kahamba akiwa amesema yeye (Mkopi) ndiye angesaidia  kupatikana kwa Dk Ulimboka ili azungumze na waandishi wa habari.
Dk Chitage alipoulizwa nini kinaendelea baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini alijibu, "Hakuna kinachoendelea."

Aliendelea, "Leo hakuna kitu, tumepumzika na hata yeye tumemwacha apumzike na familia yake," alisema Dk Chitage.

Alisema Jumuiya hiyo na familia yake wanaandaa mazingira yatakayowezesha Dk Ulimboka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari.

"Kuhusu hatua zitakazofuata tutaandaa utaratibu na tutawaarifu, juu ya hatua zipi tutachukua ikiwamo hili linaloumiza vichwa vya wengi la mazingira ya kutekwa kwake," alisema Dk Chitage.

Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rodrick Kabangila alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema yuko safarini na hajui kinachoendelea.

No comments:

Post a Comment

KARIBU