..

..
.

Thursday, August 23, 2012

Wavuta Bangi kukiona cha moto Ligi KuuMajuto Omary
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limeweka mikakati ya kuwapima wachezaji wanaovuta bangi na kutumia madawa ya kulevya katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajia kuanza mwezi ujao.

Mbali ya kuwasaka wachezaji hao, pia wataendesha zoezi la kuwasaka wachezaji wa aina hiyo katika timu ya Taifa na wale watakaogundulika watachukuliwa hatua kali.

Akizungumza jijini jana Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema wameamua kuwa wakali ili kuthibiti vitendo vya baadhi ya wachezaji wanaojiusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kuwa wameandaa utaratibu wa kuwapima wachezaji mara kwa mara katika mechi mbalimbali za ligi ili kuwabaini wachezaji hao.

Alifafanua kuwa vitendo vya uvutaji bangi na kutumia dawa za kulevya vinapigwa vita dunia nzima na sio suala la kuliacha likiendelea huku likifumbiwa macho.

“Hatuna haja ya kuficha suala hili, wale watakao bainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa kanuni,” alisema Tenga.

Alisema kuwa pamoja na kutokuwa na majina ya wachezaji wanaojihusisha na vitendo hivyo, wameona bora kutoa tamko mapema ili wale ambao wanatumia na wenye mpango wa kuanza kutumia waachane na tabia hiyo.

Tenga alitoa rai kwa viongozi wa klabu kuanza kupigia kelele suala hilo kwani mbali ya kuathiri wachezaji, pia linaathiri maendeleo ya soka hapa nchini.

“Nimemwambia mkurugenzi wa mashindano (Saad Kawemba) kuandaa utaratibu wa kuendesha zoezi la kupima wachezaji, naamini atamaliza kabla ya kuanza kwa ligi, adhabu gani watapewa wachezaji, zitatangazwa hapo baadaye,” alisema Tenga.

Alisema kuwa mchezo wa soka unastahili kuheshimiwa kutokana na kuwa na mashabiki wengi duniani na hivyo vitendo vya hujuma kama vya kutumia madawa na uvutaji wa bangi havikubaliki.

Katika hatua nyingine; Tenga alisema kuwa wameamua kuwapa mamlaka ya kusimamia Ligi Kuu ya Tanzania Bara umoja wa klabu ili kupunguza majukumu ya shirikisho.

Alisema kuwa TFF ina majukumu mengi na kulazimika kuunda kamati mbalimbali ambazo lengo kubwa ni kusaidia ufanisi wa shughuli zake.

Alifafanua kuwa katika mkutano mkuu wa 2010 walipokea hoja za klabu kutaka kuwa na chombo huru cha kusimamia ligi hiyo kama ilivyo katika nchi mbali mbalimbali duniani.

“Wakati ule mchakato ulikuwa bado na kuahidi kulifanyia kazi katika mkutano unaofuata, ambapo hoja hiyo iliwasilishwa tena na hatimaye mkutano mkuu wa mwezi Aprili mwaka huu ukatoa mamlaka kwa kamati ya utendaji kuamua suala hilo na kamati kupitisha,” alisema Tenga.

Alisema kuwa kwa vile mpira wa miguu duniani unasimamiwa na chama au shirikisho la mpira, TFF iliwapa maelekezo umoja wa klabu nini cha kufanya ili kuwa na mfumo sahihi unaokubalika kimataifa katika kusimamia ligi.

“Nashukuru klabu walikubali kufuata mfumo huo na kuomba muda wa kujipanga ili kukamilisha maelekezo yake, naamini ndani ya wiki hii watafanya hivyo na hatimaye kuanza kazi,” alisema Tenga.

Hata hivyo taarifa zilizoifikia Mwananchi jana zilisema kuwa umoja wa klabu umeshindwa kukamilisha maelekezo hayo na kuomba usimamizi wa pamoja wa ligi hiyo na kamati ya TFF.

Sababu kubwa ni muda na jinsi ya kuendesha mchakato huo ambao unahitaji umakini mkubwa ili kuweza kufikia kiwango kinachotakiwa.

No comments:

Post a Comment

KARIBU