Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Syria ulioundwa hivi karibuni, 
leo wanatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William
 Hague mjini London.
 
Kulingana na shirika la utangazaji la BBC, Mkuu wa muungano huo wa 
Upinzani nchini Syria, Ahmed Moaz al-Khatib, pamoja na wanachama wengine
 watatu wa muungano huo wanatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje 
wa Uingereza William Hague. Uingereza inania ya kuutaka muungano huo 
kuweka wazi mpango wao juu ya kipindi cha mpito nchini Syria.
Uingereza imesema pindi tu muungano huo utakapofanya hivyo, basi 
itatilia maanani swala la kuwatambua rasmi kama muungano halali wa 
upinzani kwa utawala wa rais Bashar Al Assad. Tayari Ufaransa, Uturuki 
na mataifa ya eneo la Guba yanautambua rasmi muungano huo wa upinzani.
 Wanachama wa muungano mpya wa upinzani, Syria
Wanachama wa muungano mpya wa upinzani, Syria
 
Huku hayo yakiarifiwa ndani ya Syria kwenyewe, wanaharakati wa 
upinzani wanasema vikosi vya serikali vimeanza kulishambulia eneo 
linalokaliwa na waasi la al Rastan mjini Homs. Mashambulizi mengine 
yameripotiwa katika mji wa al-Zabadani nje kidogo ya mji mkuu Damascus. 
Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria lililo na 
makao yake mjini London, takriban watu 140 wameuwawa katika mashambulizi
 ya jana pekee.
Kwa upande mwengine Ufaransa imesema itazungumza pamoja na wanachama 
wengine 27 wa Umoja wa Ulaya juu ya pendekezo la kupunguza vikwazo vya 
silaha vya Umoja huo ambavyo kwa sasa vinazihusu pande zote mbili 
zinazohusika na vita vya Syria. Lakini Urusi imesema hatua yoyote ya 
aina hiyo itakuwa ni kukiuka sheria ya kimataifa .
 Jengo moja likiwaka moto nchini Syria
Jengo moja likiwaka moto nchini Syria
 
Kwa Upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius 
amesema hatua ya waasi kupewa silaha ni njia moja ya kuwalinda kutokana 
na mashambulizi makali yanayofanywa na vikosi vya serikali ya Assad.
"Hakuna haja ya kuupa sura ya kijeshi mzozo huu. Lakini haikubaliki pia 
kuona maeneo yaliyokombolewa,yanashambuliwa kwa mabomu. Lazima pawepo 
wizani,na si rahisi. Kwa upande mmoja kutoingilia upande wa kijeshi na 
upande wa pili kuzuwia maeneo yaliyokombolewa yasibomolewe. Ndio maana 
suala la kupelekwa silaha za kujilinda linabidi lizushwe hapa." amesema 
Laurent Fabius
Umoja wa Mataifa walalamika
Wakati huo huo kwa mujibu wa barua iliyolifikia shirika laahabari la AFP
 hapo jana Umoja wa mataifa umelalamika kwa serikali ya Syria kwa kudai 
kwamba ilikuwa na ruhusa ya umoja huo kuwashambulia waasi katika eneo la
 milima ya Golan ambalo halipaswi kuwa na harakati zozote za kijeshi.
 Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia amani Herve Ladsous
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia amani Herve Ladsous
 
Katika barua iliotumwa kwa balozi wa Syria, Mkuu wa Umoja huo 
anayeshughulika na swala la amani Herve Ladsous, aliitaka Syria 
kusimamisha mashambulizi hayo mara moja katika maeneo hayo ya kijeshi 
yalio kati ya Syria na Israel ambayo huenda yakahatarisha maisha ya raia
 pamoja na waangalizi wa Umoja wa Mataifa walioko huko. 
Tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria miezi 20 iliopita tariban watu 39,000 wameuwawa
 
No comments:
Post a Comment